Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Adolf Mkenda
Na Mathias Canal,Morogoro.
SERIKALI imesema kuwa inaendelea kufanya mapitio ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 na mabadiliko ya mitaala ili kuongeza ubora wa elimu na mafunzo.
Katika Mapitio hayo ya mitaala na sera pia yanaangazia kwa karibu Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima ili wakati utatuzi wa changamoto ukiendelea serikali kuangalia nini kifanyike ili kuboresha elimu ujuzi kwa wanafunzi ikiwemo watu wazima.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda ameyasema hayo leo tarehe 9 Septembà a 2022 wakati wa hafla fupi ya ufungaji wa mafunzo ya Baraza la Usimamizi wa Taasisi ya elimu ya watu wazima (TEWW) Kampasi ya Morogoro.
Prof Mkenda amesema kuwa Taasisi hiyo inapaswa kushiriki kikamilifu katika utoaji wa maoni ikiwa ni pamoja na kushirikisha kwa karibu wadau wengine kutoa maoni namna ya kuboresha taasisi hiyo hususani katika maeneo ya ujuzi.
Pia, Prof Mkenda amesema kuwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa kuhusu kuhakikisha kuwa watanzania waliokosa fursa ya kusoma kutokana na matatizo mbalimbali wanapata fursa ya kuendelea na masomo.
Serikali itaendelea kuisaidia Taasisi ya elimu ya watu wazima ili kuratibu na kusimamia vyema urahisi wa wananchi kupata fursa ya elimu, hivyo ili kukamilisha jambo hilo itaendelea kuimarisha miundombinu ikiwemo ukarabati na ujenzi wa majengo ya taasisi.
"Majengo ni muhimu lakini Elimu sio majengo pekee tunaweza kutumia muda mrefu kwenye majengo, serikali italeta hela kwa ajili ya majengo lakini kama hatukuweka weledi kwa watu hatuwezi kufika" Amekaririwa Waziri Mkenda
Waziri Mkenda amemtaka Mwenyekiti wa Baraza hilo pamoja na wataalamu kufanya ziara nchini Ujerumani ili kujionea namna Taasisi ya elimu ya watu wazima nchini humo inavyofanya kazi ili kuongeza ufanisi na uwajibikaji.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la usimamizi wa (TEWW) Dkt Naomi Katunzi amempongeza waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe Prof Adolf Mkenda kwa usimamizi madhubuti wa baraza hilo pamoja na mabadiliko makubwa ya iutendaji yanayofanyika katika wizara.
Amesema kuwa Mafunzo hayo yanayotolewa chini ya Chuo cha Uongozi pamoja Ofisi ya Msajili wa hazina yamejikita katika kuwaongezea ufanisi wa kiutendaji na uwajibikaji serikali ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kuwa wanaacha alama na kielelezo bora katika uwajibikaji.
Mwenyekiti huyo amezitaja changamoto zinazoikabili taasisi hiyo kuwa ni pamoja na ukarabati wa majengo chakavu ikiwa sambamba na ujenzi wa majengo mapya kwa ajili ya ofisi.
Social Plugin