Kamanda wa polisi mkoa Kigoma Filemon Makungu (wa pili kushoto) akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusiana na kuuawa kwa watu wawili na wengine sita kujeruhiwa na wafugaji katika kijiji cha Mvinza wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WATU wawili wamekufa na wengine sita kujeruhiwa baada ya watu wanaoaminika kuwa wafugaji kuvamia kambi ya Wakala wa huduma za misitu Tanzania (TFS) kwenye kijiji cha Mvinza wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma.
Kamanda wa polisi mkoa Kigoma,Filemon Makungu akizungumza na waandishi wa habari mjini Kigoma leo amesema kuwa uvamizi huo ulifanyika kwenye kambi hiyo iliyopo kwenye hifadhi ya msitu wa Makere Kusini mkoani Kigoma mwishoni mwa wiki iliyopita.
Kamanda Makungu aliwataja waliokufa kuwa ni pamoja na Mkazi wa kijiji cha Mvinza aliyejulikana kwa jina moja la Salvatory ambaye alikuwa kibarua kwenye shamba hilo la miti la TFS ambaye alichomwa na vitu vyenye ncha kali na kufariki dunia wakati wa uvamizi huo.
Aidha alisema kuwa jana polisi wakiwa kwenye ukaguzi wa eneo hilo kuangalia athari ya tukio hilo maiti ya mtu mwingine ilipatikana ambaye alitambulika kwa jina la Thomas Alfred aliyekuwa akifanya kazi za vibarua kwenye kambi hiyo ya TFS mwili wake ukiwa na majeraha makubwa shingoni.
Aliwataja waliojeruhiwa kwenye tukio hilo kuwa ni pamoja na Dora Nicolaus na David Lazaro ambao ni watumishi wa Suma JKT wakiwa kwenye kazi ya ulinzi ya kambi hiyo, Amon Moshi Mtunza Bustani, Ndayishimiye Haruna Mkulima wa bustani na Elcado Enos Mkulima.
Sambamba na mauaji na watu hao kujeruhiwa pia vitu mbalimbali vimeteketezwa kwa moto likiwemo trekta mali ya TFS,nyumba moja ya tofali za kuchoma iliyoezekwa na bati ikitumika kama ofisi, pikipiki sita za watuhumiwa waliokamatwa kwa kuingia kwenye hifadhi yam situ kinyume cha sheria, gunia 20 za maharage, gunia 70 za mahindi, gunia 30 muhogo na gunia 20 za mtama.
“Taarifa za awali zinaonyesha kuwa siku za karibuni kuna ng’ombe ambao idadi bado haijajulikana ya wafugaji walikamatwa na kuchukuliwa na maafisa wa TFS kwa tuhuma za ng’ombe hao kuingizwa kwenye hifadhi ya msitu kwa ajili ya malisho, hivyo vurugu hizo zimekuja kama nia ya watu hao kulipiza kisasi kwa mifugo yao kukamatwa na ndiyo maafa hayo yametokea,”alisema Kamanda Makungu.
Hadi sasa watu watatu ambao wanaaminika ni sehemu ya wafugaji hao wamekamatwa na wanashikiliwa na polisi wakituhumiwa kuhusika na tukio hilo na kwamba uchunguzi zaidi unaendelea kuhusiana na tukio hilo.
Social Plugin