Watoto wanne wa familia moja, wamefariki dunia baada ya nyumba walimokuwa wamelala kuteketea kwa moto.
Tukio hilo limetokea majira ya saa 6:30 usiku wa kuamkia Jumamosi Septemba 24,2022 katika makazi ya watu yaliyopo ndani ya eneo la mgodi wa Mwadui,wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
Watoto waliopoteza maisha kutokana na tukio hilo, ni Cecilia Richard mwenye umri wa miaka 14, aliyekuwa akisoma darasa la saba katika shule ya msingi Mwadui (C) Clarence Richard mwenye umri wa miaka 6, aliyekuwa akisoma darasa la kwanza katika shule ya msingi Mwadui (A) Thadeo Richard mwenye umri wa miaka 3 na Aisha Ashraf mwenye umri wa miaka 6 aliyekuwa akisoma darasa la kwanza katika shule ya awali na msingi Mwenge Manispaa ya Shinyanga.
Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga, limesema chumba walichokuwa wamelala watoto wanne waliofariki dunia baada nyumba yao kushika moto huko Mwadui Wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, kilikuwa na jumla ya watoto saba.
Kaimu Kamada wa Polisi mkoa wa Shinyanga Jackson Mwakagonda, amesema watoto watatu kati yao waliokolewa, lakini walilazwa katika Hospitali ya Mwadui kwa matibabu, baada ya kujeruhiwa kwa moto , ambao pia ulimjeruhi baba wa familia hiyo Richard Dominick Mhoja (37) wakati akijaribu kuwaokoa watoto wengine.
Taarifa zaidi zinabainisha kuwa, nyumba hiyo wakati akishika moto wazazi hawakuwepo nyumbani, ambapo baada ya kupewa taarifa walirudi na baba (Richard Mhoja) aliungana na majirani wakavunja dirisha na kufanikiwa kuwaokoa watoto watatu kati ya saba waliokuwa wamelala katika chumba hicho, lakini kwa wale wengine wanne hawakufanikiwa kutokana na kuzidiwa na moto, na hivyo wakateketea ndani ya nyumba.
Watoto waliookolewa katika ajali hiyo ni Joseph Richard mwenye umri wa miaka 9, Abel Richard mwenye umri wa miaka 5 na Azirat Ashraf mwenye umri wa miaka 3.
Waliopoteza maisha kutokana na tukio hilo, ni Cecilia Richard mwenye umri wa miaka 14, aliyekuwa akisoma darasa la saba katika shule ya msingi Mwadui (C) Clarence Richard mwenye umri wa miaka 6, aliyekuwa akisoma darasa la kwanza katika shule ya msingi Mwadui (A) Thadeo Richard mwenye umri wa miaka 3 na Aisha Ashraf mwenye umri wa miaka 6, anayeelezwa kuwa alikuwa akisoma darasa la kwanza katika shule ya msingi Mwenge iliyopo Manispaa ya Shinyanga, ambaye alikuwa ni mgeni katika familia hiyo.
Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, chanzo cha moto huo kinatokana na uzembe wa watoto kuacha jiko la umeme likiwaka, ingawa baadhi ya majirani walioshuhudia tukio hilo wanadai kuwa, moto huo unatokana na dawa ya mbu waliyokuwa wamewasha watoto hao muda mfupi kabla ya kulala, kwa sababu umeme katika nyumba hiyo haukukatika na badala yake uliendelea kuwaka kama kawaida ikiwemo taa za nyumba, wakati nyumba hiyo ikiteketea kwa moto.
Social Plugin