Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MPANGO WA NYP+ WAZINDULIWA KUKABILIANA NA VVU

 
Naibu katibu Mkuu,Ofisi ya waziri mkuu sera, uratibu na Bunge Kasper Mmuya akizungumza kwenye uzinduzi wa NYP+

Na Dotto Kwilasa,DODOMA.

NAIBU katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu na Bunge Kasper Mmuya ameitaka tume ya kudhibiti ukimwi nchini TACAIDS  kuja na mifumo mizuri ya ugawaji kondomu ili kudhibiti changamoto ya uhaba wa kondomu nchini unaotokana na baadhi ya watu wachache kuzichukua kwa wingi na kuzitumia isivyo sahihi.

Mmuya amesema  hayo  Jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa mpango mkakati wa mtandao wa vijana wanaoishi na VVU nchini (NYP+)  ambapo amesema hakuna sababu ya kuwepo uhaba huo kutokana na kuwa kondomu zinazoingia nchini ni nyingi na zinazoweza kukidhi mahitaji yaliyopo.

Amesema katika juhudi za kutokomeza maambukizi ya virusi vya ukimwi vijana wanatajwa kuwa kundi muhimu kufikiwa , kutokana na kundi hili kuwa kundi  linaloongoza katika kupata maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi.

"Katika kuendelea mapambano lazima juhudi zifanyike kulifikia kundi hili, kupitia mpango mkakati wa mtandao wa vijana wanaoishi na VVU nchini NYP+, lazima  changamoto ziishe na kuanzisha mafanikio ambayo yameshafikiwa  katika kukabiliana na  maambukizi ya VVU na Ukimwi,"amesema

Katika hatua nyingine amewataka vijana wanaoishi na Virusi vya Ukimwi(VVU)nchini kuendeleza mapambano dhidi ya Virusi hivyo  ili kuondokana na maambukizi mapya yatakayoweza kukatisha ndoto zao.

Amesema pamoja na mafanikio yaliyopo ni vyema kuongeza jitihada katika kuhamasisha upimaji wa VVU ili  kufikia malengo ya Kitaifa ya 95 kwa mwaka  2025 na ifikapo mwaka 2030 iwe imefikia sifuri (0 ).

“Nitoe wito kwa wadau wote wanaotekeleza afua za mwitikio wa UKIMWI kufanya tathimini ya mwelekeo wa utekelezaji katika kufikia malengo  ili palipo na changamoto tuweze kurekebisha na kuimarisha na penye mafanikio tuongeze nguvu na Mipango yetu ya kimkakati ionyeshe wazi jinsi tutakavyofikia Tanzania isiyo na UKIMWI ifikapo mwaka 2030,”amesema Naibu Katibu Mkuu huyo.

Amesisitiza kuwa kupitia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ambao ni waratibu wa shughuli za UKIMWI ndani ya mikoa wawe chachu ya utekelezaji wa maelekezo hayo ndani ya mikoa yao.
 
“Niwasisitize watumishi wa Serikali kupitia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mkasimamie na kuratibu vyema Halmashauri zote kwa kushirikiana na Tume ya Taifa ya Kudhibiti UKIMWI (TACAIDS) tuweze kutimiza vyema azma yetu,”amesisitiza.

Aidha amesisitiza  Uhamasishaji kwa wanaume kuhakikisha wanatumia huduma za VVU na upimaji kwa ajili ya kufikia 95 ya kwanza pamoja na kufuatilia vijana wakike watumie  huduma za VVU ili kuhakikisha wanatimiza ndoto zao na kutokomeza ukatili wa kijinsia.

Mwenyekiti wa NYP+,Pudensia Mbwiliza  amesema asilimia arobaini ya maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi nchini yanatajwa kuwakabili vijana wenye umri wa kuanzia miaka 18 hadi 28 huku wasichana wakiwa ni asilimia themanini ya kundi hilo na kusisitiza kuwa wako tayari kuendelea kushirikiana na serikali kulifikia kundi la vijana na kuliwezesha kukabiliana na maambukizi ya VVU.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com