Mkazi mmoja wa wilayani Handeni mkoani Tanga Mariam Mbwana (35) amekutwa amefariki katika nyumba ya kulala wageni huku mwanaume aliyekuwa naye akitorokea kusikojulikana.
Akielezea tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia Jumamosi Septemba 24, 2022 meneja wa nyumba ya kulala wageni Paradise, Christian Masawe amesema alifika mwanaume ambae hakutambulika na kulipia chumba hicho.
Amesema kuwa mteja huyo wa kiume kabla ya kuingia kulala alipata huduma ya chakula na vinywaji na alikuwa peke yake na wala hawakufahamu kuwa alikuwa na mwenzake.
Ameongeza kuwa asubuhi wakati mfanyakazi anakwenda kukagua chumba kwaajili ya kufanya usafi, ndio akagundua upo mwili wa mwanamke amefariki dunia na kutoa taarifa kwa uongozi.
"Aliyekuja kuchukua chumba ni mwanaume na alikuja peke yake yule mwanamke haijulikani aliingia saa ngapi majira ya usiku, ila mwanaume huyo alikula na kunywa akiwa peke yake na inaonekana alitoka asubuhi na kumuacha ndani",amesema Massawe.
Mdogo wake marehemu Maimuna Seleman amesema alikuwa na marehemu mpaka saa mbili usiku na baadae kila mmoja alikwenda kwake, ila ilipofika saa tatu usiku watoto walikwenda kumwambia kuwa hawamuoni mama yao.
"Jana kashinda vizuri hata sijui imekuwaje, mpaka saa mbili usiku mimi niliondoka na kwenda kwangu ila asubuhi ndio nikapigiwa simu na kuambiwa tukio hili ila sijui kimetokea nini",amesema Maimuna.
Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama na Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Siriel Mchembe amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataka wananchi kutoa ushirikiano ili abainike mwanaume aliyefanya tukio hilo.
"Niagize wananchi mjitahidi mnapoingia na mtu kwenye nyumba za wageni mhakikishe mnajiandikisha kwenye daftari la wageni, lengo linapotokea tukio kama hilo ili mmoja aweze kutambuliwa",amesema Mchembe.
Social Plugin