Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI IMETENGA BILIONI 100 UJENZI VYUO VYA VETA NCHINI.

 

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia  Prof Adolf Mkenda

Na Mathias Canal, DODOMA.

SERIKALI imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 100 kwa  ajili ya ujenzi wa vyuo vya Ufundi Stadi katika kila Mkoa na Wilaya nchini kwa mwaka wa fedha 2022/2023. 

Kiasi hicho cha fedha ni kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Vyuo vya Ufundi Stadi katika Wilaya 62 kwa Wilaya ambazo zilikuwa hazijajengewa Vyuo vya Ufundi Stadi.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia  Prof Adolf Mkenda amesema hayo leo tarehe 21 Septemba 2022 Bungeni Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Dkt. Pius Stephen Chaya, Mbunge wa Jimbo la Manyoni Mashariki aliyetaka kufahamu serikali ina Mpango gani wa kujenga Chuo cha VETA Wilayani Manyoni.

Aidha, akijibu swali hilo amesema Wilaya ya Manyoni ni miongoni mwa Wilaya hizo 62 ambazo zipo kwenye mpango wa kujengewa Vyuo vya Ufundi Stadi kwa mwaka huu wa fedha.

Waziri Mkenda pia amewashauri wananchi wa wilaya ya Manyoni wakiwemo wa Jimbo la Manyoni Mashariki waendelee kutumia  Chuo cha Ufundi Stadi cha Mkoa wa Singida, na Chuo cha Wilaya ya Ikungi, Pamoja na Vyuo vya Singida na Msingi FDC  na Vyuo vingine vya ufundi stadi vilivyopo nchini. 


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com