Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUTATHMINI UPYA MIPAKA YA MAPORI YA AKIBA YALIYOPANDISHWA HADHI



***********************

Serikali imejipanga kutathmini upya Mapori ya Akiba ya Luganzo-Tongwe, Igombe, Wembere, Inyonga na Ugalla ili kutatua changamoto ya muingiliano wa mipaka yenye hadhi tofauti na kupelekea baadhi ya maeneo ya Mamlaka za Serikali za Mitaa vikiwemo Vijiji na maeneo mengine kuingizwa ndani ya mapori hayo.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) alipokuwa akitoa tamko la Serikali katika ukumbi wa Manispaa ya Mpanda Mkoani Katavi.

“Hii ni mojawapo ya utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwamba tupunguze taharuki na migongano kati ya wananchi na maeneo ya hifadhi” Mhe. Masanja amesisitiza.

Amesema mipaka mipya ya Pori la Akiba Igombe imepishana na kusababisha malalamiko kwa wananchi kwa kuwa kuna sehemu imemega maeneo ya vijiji ambayo yanatumika kwa ajili ya kilimo na makazi Serikali.

Kuhusu Pori la Akiba Luganzo Tongwe Mhe. Masanja amefafanua kuwa mipaka yake imechukua maeneo mengine ya ziada yakiwemo Hifadhi ya Msitu wa Mpanda line, Hifadhi ya Msitu wa Tongwe West, Sehemu ya Hifadhi ya Msitu wa Masito, Eneo la Makazi ya Wakimbizi la Mishamo, sehemu ya maeneo ya vijiji katika kata ya Mishamo (Kijiji cha Kapemba), na vijiji vya Nguruka, Malagarasi na Itebula.

Ili kutatua changamoto hiyo Serikali imeamua kuanzisha upya mchakato wa uanzishwaji wa Pori la Akiba Luganzo – Tongwe kwa kushirikisha Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi, Mamlaka za Serikali za Mitaa (Tabora, Katavi na Kigoma), Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA).

Aidha, katika Pori la Akiba Ugalla Serikali imeamua kuondolewa kwa Hifadhi ya Msitu wa Walla River kwenye mipaka ya Pori la Akiba Ugalla na kwamba utaendelea kusimamiwa na Halmashauri ya wilaya ya Sikonge.

Pia, amesema Pori la Akiba Wembere Serikali itatuma wataalam kutoka Wizara za Ardhi, Maliasili na Utalii na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kuandaa ramani ya Pori la Akiba Wembere lenye ukubwa wa kilomita za mraba 5,385.81 litakalotanda kwenye eneo la Bonde la Ardhi Oevu la Wembere kwenye wilaya za Igunga, Uyui, Sikonge na Manyoni kwenye mikoa ya Tabora na Singida kama ilivyokusudiwa tangu awali na kutamkwa kwenye Tangazo la Serikali. Na. 456 la tarehe 25/06/2021.

Mhe. Masanja ametoa rai kwa wananchi kuheshimu maeneo yatakayoainishwa kwa ajili ya uhifadhi na pia amewataka wawe wadau wa uhifadhi kwani wao ni wanufaika wakuu kwa kuwa uhifadhi unasaidia kutunza vyanzo vya maji, mazingira na kuondoa ukataji wa miti .



Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com