Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA YAPATIWA TSH.TRILIONI 2 ILI KUTEKELEZA MIRADI YA KIMAENDELEO

 

Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba (kulia) na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Kim Sun Pyo, wakisaini mikataba ya mikopo nafuu ya jumla ya dola za Marekani bilioni moja sawa na shilingi trilioni 2.3 kutoka Mfuko wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Korea (EDCF) kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba (kulia) na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Mhe. Kim Sun Pyo, wakionesha hati ya mikopo nafuu ya jumla ya dola za Marekani bilioni moja sawa na shilingi trilioni 2.3 kutoka Mfuko wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Korea (EDCF) kwa ajili kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, jijini Dar es Salaam.

Katibu Mkuu  Afisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil akizungumza baada ya aada ya kumalizika kwa hafla ya utiaji saini mikopo nafuu ya jumla ya dola za Marekani bilioni moja sawa na shilingi trilioni 2.3  kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo

Picha ya pamoja
...................................

NA MUSSA KHALID,DAR ES SALAAM 

Serikali imesaini makubalino na serikali ya Jamhuri ya Korea mkopo nafuu wa Dola Bill 1 sawa na Tsh.Trilioni 2.3 kutoka mfuko wa ushirikiano wa kiuchumi wa Maendeleo ya Korea (EDCF) kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.

Hafla ya utiaji saini imefanyika leo jijini Dar es salaam baina ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Emannuel Tutuba pamoja na Balozi wa Serikali ya Jamhuri ya Korea Kim Sun Pyo.

Akizungumza katika hafla hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Emmanuel Tutuba amesema kuwa baadhi ya miradi ambayo itatekelezwa ni pamoja na Mradi wa Upanuzi wa Mfumo wa Vitambulisho vya Taifa awamu ya pili ambao utagharimu Dola Mill 70 sawa na Bill 63.1 za kitanzania .

Aidha amesema fedha hizo zitatumika katika uboreshaji wa miundombinu ya Taifa pamoja na taarifa za ardhi kwa Dola za Kimarekani  Mill 65 zawa na Bill 151.5 za kitanzania.

‘Miradi mingine ni wa uendelezaji wa Mifumo ya Usambazaji wa Majisafi na ya Kutibu majitaka kwa dola za Marekani milioni 70 sawa na sh. bilioni 163.1 na Mradi wa Ujenzi wa Chuo cha Kisasa cha mafunzo ya Usafirishaji wa Reli kwa dola za Marekani milioni 80 sawa na sh. bilioni 186.4’amesema Tutuba

Tutuba amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, itachukua hatua zote muhimu kuhakikisha ufanisi wa utekelezaji wa miradi yote iliyofadhiliwa kwa fedha za makubaliano haya zinatumika vizuri kufikia malengo yaliyokusudiwa 

Kwa upande wake Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Tanzania Kim Sun Pyo, amesema kuwa Serikali yake   itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo kwa manufaa ya wananchi wake.

Naye Katibu Mkuu  Afisi ya Rais Fedha na Mipango Zanzibar, Dkt. Juma Malik Akil, ameishukuru Jamhuri ya Korea kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano na Tanzania kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali nchini ukiwemo  Mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Binguni Zanzibar ambayo inatarajiwa kuwa hospitali kubwa.

Hata hivyo Dkt. Akil amesema kuwa Ujenzi wa Hospitali ya Binguni utafungua fursa muhimu katika kuendeleza Sekta ya Afya nchini kwa kuwa ni sekta muhimu katika nguvu kazi na maendeleo ya nchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com