Balozi wa Singapore nchini Tanzania Douglas Foo |
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda |
Na Mathias Canal, Dar es salaam.
SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia imesema ipo tayari kubadilishana na Singapore wakufunzi wa vyuo vya Ufundi na Ujuzi ili kuongeza uelewa zaidi kwa wanafunzi.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda ameyasema hayo leo tarehe 2 Agosti 2022 wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Singapore nchini Tanzania Mhe. Douglas Foo Jijini Dar es salaam.
Waziri Mkenda amesema kuwa wakufunzi wa Tanzania wataenda nchini Singapore kujifunza namna nchi hiyo ilivyofanikiwa katika ufundi na elimu ujuzi, vilevile wakufunzi wa Singapore kutembelea vyuo vya ufundi na elimu ujuzi nchini Tanzania.
Amesema kwa pamoja wakufunzi hao watakapozuru katika nchi hizo watajadiliana kwa pamoja namna bora ya kuimarisha elimu ujuzi, ambapo amebainisha kuwa Tanzania itanufaika zaidi kwa wataalamu wa Singapore kwani nchi hiyo imefanikiwa zaidi katika sekta ya elimu ujuzi.
“Tunapoenda huko mbele elimu ya ujuzi ni lazima ipate kipaumbele kikubwa ili wanafunzi wanapomaliza iwe rahisi kujiajiri na kujipatia kipato iikiwa ni pamoja na kuweza kubadilisha maisha yao ikiwemo kuajiri watu wengine”amesema Waziri Mkenda
Naye Balozi wa Singapore nchini Tanzania Douglas Foo amesema Singapore inatarajia kuongeza ushirikiano na Tanzania katika sekta ya elimu ili kubadilishana mbinu na ujuzi kwa maendeleo ya uchumi wa viwanda.
Amesema Singapore imeendelea na uwekezaji katika teknolojia inayo rahisisha ufanyaji kazi pamoja na ufuatiliaji wa masuala mbalimbali ikiwemo masuala ya kielimu hivyo imeridhia kuunganisha uelewa wa pamoja wa wakufunzi wa ufundi na elimu ujuzi.
Social Plugin