TBS YATOA MAFUNZO KWA WAFANYABIASHARA WANAOAGIZA NA KUUZA BIDHAA ZA CHAKULA NA VIPODOZI JIJINI MWANZA


Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limetoa mafunzo kwa wafanyabiashara wanaoagiza na kuuza bidhaa mbalimbali za chakula na vipodozi jijini Mwanza ili kuwajengea uwezo kutekeleza shughuli zao kwa kuzingatia Sheria. 

Mafunzo hayo yamefanyika Alhamisi Septemba 29, 2022 yakiwashirikisha wafanyabishara mbalimbali wakiwemo waagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi, wamiliki wa maghala ya kuhifadhia bidhaa na wamiliki wa maduka makubwa ya bidhaa za jumla. 

Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya Nyamagana mkoani Mwanza Amina Makilagi amewataka wafanyabishara kuwa wazalendo kwa kuhakikisha wanaingiza nchini bidhaa zenye ubora zisizo na madhara kwa watumiaji 

Amesema Mwanza ni jiji la pili kiuchumi nchini na pia kitovu cha biashara katika nchi za ukanda wa Afrika Mashariki hivyo ni vyema wafanyabishara wakatumia fursa hiyo vizuri kwa kuhakikisha wanaagiza bidhaa zenye viwango na kuzihifadhi katika mazingira salama ili zisiharibike kabla ya kumfikia mtumiaji. 

"Serikalini inayoongozwa na Rais wetu Mhe. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha miundombi ya usafiri na usafirishaki ikiwemo ujenzi wa meli mpya katika Ziwa Victoria, bandari kavu ya Fela, reli ya kisasa (SGR) hadi jijini Mwanza na uboreshaji wa uwanja wa ndege wa Mwanza ili kurahisisha shughuli za kibiashara" amesema DC Makilagi. 

Katika hatua nyingine, Makilagi ameonya kuwa wafanyabishara wanaouza bidhaa zenye viambata sumu wanaliangamiza taifa na wanaenda kinyume na lengo la Serikali ya kuhakikisha afya ya wananchi iko salama akisema tafiti mbalimbali zinazoendelea kufanyika zinaonyesha magonjwa kama kansa yanasabanishwa na ulaji wa vyakula pamoja na utumiaji wa vipodozi vyenye viambata sumu. 

Pia Makilagi ameipongeza TBS kwa kuendelea kutoa elimu na semina kwa wadau mbalimbali ili kutambua bidhaa zenye ubora na zile zenye viambata sumu zilizopigwa marufuku akisema kila mdau anapaswa kutimiza wajibu ili jamii iwe salama. 

Naye Meneja wa TBS Kanda ya Ziwa, Mhandisi Joseph Mwaipaja amesema Shirika hilo litaendelea kuchukua hatua kali za kisheria kwa wafanyabishara wanaoingiza sokoni bidhaa zilizopigwa marufuku ingawa kabla ya kuchukua hatua hizo TBS inawaelimishwa kwanza. 

Kwa upande wake mmoja wa wafanyabiashara walioshiriki mafunzo hayo, Mohamed Muhan amesema watazingatia elimu waliyoipata ikiwemo kuagiza na kuuza bidhaa zilizosajiliwa kusajiliwa kisheria ili kwa pamoja kwa kushirikiana na TBS wafanikishe jitihada za kuondoa sokoni bidhaa zenye viambata sumu. 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post