TBS YAWAFIKIA WANANCHI 5,446 MKOANI MWANZA


Mkaguzi ( TBS), Bw. Nelson Mugema akitoa elimu kuhusu umuhimu wa kununua bidhaa zilizothibitishwa ubora na usalama wake na TBS sambamba na kuzingatia muda wa mwisho wa matumizi wa bidhaa kwa wananchi waliokuwepo katika gulio la Kisesa,wilayani Magu, wakati wa kampeni ya elimu kwa umma katika ngazi ya wilaya mkoani Mwanza. Meneja Uhusiano na Masoko ( TBS) Bi. Gladness Kaseka akitoa elimu kwa wananchi waliohudhuria mnada wa Bungulwa Wilayani Kwimba kuhusu umuhimu wa kusoma taarifa zilizopo katika bidhaa sambamba na kuzingatia muda wa mwisho wa matumizi.Maafisa wa TBS wakitoa elimu kwa wananchi kuhusu majukumu ya Shirika pamoja na namna ya kutuma maoni/malalamiko pale wanapokutana na changamoto kwenye bidhaa katika mnada wa Misasi wilayani Misungwi mkoani Mwanza. Maafisa wa TBS wakitoa elimu kwa wajasiriamali wanawake wa wilaya za Sengerema, Kwimba,Ilemela na Magu mkoani Mwanza . Wajasiriamali hao walielimishwa juu ya taratibu za kupata leseni ya kutumia alama ya ubora katika bidhaa zao na faida za kuthibitisha ubora wa bidhaa zao ikiwa ni pamoja na kupata masoko kiurahisi ndani na nje ya Nchi. Jumla ya wajasiriamali 96 walifikiwa katika kampeni ya elimu kwa umma ngazi ya wilaya iliyofanyika kuanzia tarehe 05.09.2022 mpaka tarehe 19.05.2022.

**************************

WATU 5, 446 miongoni mwao wakiwemo Wanawake wajasiriamali 96 katika wilaya tano za Mkoa wa Mwanza wamepatiwa elimu kuhusu masuala mbalimbali kuhusu viwango na taratibu za kufuata ili kupata alama ya ubora hususan kwa wajasiriamali.

Elimu hiyo kwa umma ilitolewa na maofisa wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuanzia Septemba 5 hadi 19, mwaka huu katika Wilaya za Sengerema (Soko Kuu la Sengerema), Kwimba (mnada wa Bungulwa), Misungwi (Mnada wa Misasi), Ilemela (Gulio la Kitangiri) na Magu (Gulio la Kisesa).

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Mwanza wakati akitoa majumuisho ya elimu hiyo kwenye wilaya hizo tano,Meneja Uhusiano na Masoko wa TBS, Bi. Gladness Kaseka, alisema kwa kipindi hicho walitoa elimu kwa umma kuhusiana na majukumu ya shirika hilo pamoja na ile inayohusiana na masuala mbalimbali udhibiti ubora kwa ujumla.

"Kupitia elimu hii tumeweza kufikia jumla ya watu 5, 446 na tuliwafuata kule waliko wanakofanyia shughuli zao ikiwemo kwenye masoko, minada, magulio na maeneo mengine yenye mikusanyiko ya watu wengi,"alisema Kaseka.

Kwa upande wa wajasiriamali, Kaseka alisema waliweza kutoa elimu hiyo kwa wajasiriamali wengi wakiwemo wanawake 96 wa mkoa huo (Mwanza).

"Wajasiriamali tumewafundisha taratibu za kufuata ili kupata leseni ya kutumia alama ya ubora na jinsi inavyoweza kuwasaidia kupata masoko ya ndani na nje ya nchi," alisema Kaseka.

Kwa upande wa wananchi, Kaseka alisema pamoja na mambo mengine waliwafundisha umuhimu wa kununua bidhaa zilizothibitishwa na TBS, umuhimu wa kuangalia tarehe ya mwisho wa matumizi kwa bidhaa wanazotaka kuzinunua na jinsi kuwasiliana na TBS wanapokuwa na maoni au kukutana na changamoto zozote.

Kwa mujibu wa Kaseka, Wananchi waliopata elimu hiyo waliahidi kuhakikisha wanakuwa mabalozi kwa kuhamasisha jamii kutumia bidhaa zilizothibitishwa ubora na shirika hilo pamoja na kuwa makini kuagalia muda wa mwisho wa matumizi wa bidhaa wanazotaka kuzinunua.

Aidha, alisema kupitia elimu hiyo walitoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa TBS pindi wanapokutana na bidhaa zilizokwisha muda wake wa matumizi au wanapotilia shaka bidhaa yoyote katika soko.

Kwa upande wa wananchi waliopatiwa elimu hiyo, walipongeza hatua hiyo ya TBS, wakisema itakuwa mwarobaini wa changamoto wanazokuwa wakikutana nazo. Mmoja wa wajasiriamali waliopatiwa elimu hiyo akizungumza kwa sharti la majina yake kutochapishwa gazetini, alipongeza TBS kwa kuwaelimishwa taratibu za kufuata ili kuthibitisha ubora bidhaa anazozalisha.

Alisema wanapopeleka bidhaa zao sokoni kama bidhaa hajathibitishwa na TBS wanakabiliwa na changamoto ya kupata masoko, hivyo elimu waliyoipata imewafungulia milango ya kuanza mchakato wa kuthibitisha ubora wa bidhaa zao, haswa ukizingatia hakuna gharama zozote kwa miaka mitatu ya mwanzo.

"Kwa sasa wananchi wengi wana elimu ya viwango, tukiwa sokoni tunaulizwa kama bidhaa zetu zina TBS (alama ya ubora) sasa tunaanza safari ya kutafuata alama ya ubora," alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post