*************************
WAFANYABIASHARA wanaokuja kufanya biashara pamoja na kuwekeza nchini, wametakiwa kuzingatia taratibu zilizowekwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kuepuka vikwazo vya kibiashara wanavyoweza kukumbana navyo.
Ushauri huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Afisa Masoko wa TBS, Deborah Haule, wakati akizungumza na washiriki waliotembelea banda la shirika hilo kwenye Maonesho ya Biashara ya Afrika Mashariki yaliyofanyika Diamond Jubilee, jijini Dar es Salaam kuanzia Septemba 22 hadi 24, mwaka huu.
Kwa upande wa wafanyabiashara wa biadhaa ambao walihudhuria maonesho hayo kutoka nchi za Afrika Mashariki, Haule alisema walielimishwa jinsi mashirika ya viwango ya nchi hizo yalivyo na makubaliano ya pamoja, ambapo mfanyabiashara kutoka nchi mojawapo anapopeleka bidhaa yake nchi nyingine ikiwa na alama ya ubora ya shirika la nchi husika, basi bidhaa yake haiwezi kupimwa tena kwa ajili ya kuithibitisha ubora.
Alisema mashirika ya viwango ya nchi hizo za Afrika Mashariki yaliingia makubaliano hayo ili kuwaondolea vikwazo vya kibiashara wafanyabiashara, hivyo ni muhimu kuhakikisha bidhaa zao zina alama ya ubora kutoka mashirika ya nchi husika.
''Hii imelenga kurahisisha ufanyaji biashara katika nchi za Afrika Mashariki,'' alisema Haule.
Kwa upande wa wafanyabiashara ambao wanafanya biashara kutoka nje ya nchi za Afrika Masharik, Haule alisema;
''Kwa wanaoleta bidhaa za chakula na vipodozi cha kwanza wanachotakiwa kufanya ni kusajili bidhaa zao za chakula au vipodozi kupitia tovuti ya TBS, ambapo wakishaingia kwenye mfumo, utawasaidia namna ya kujaza taarifa zao pamoja na kulipia gharama zinazotakiwa.
Baada ya hapo wataleta sampuli tutazipima,''alisema Haule na kuongeza; ''Wakishapatiwa huo usajili, hatua inayofuatia pale wanapoleta mzigo taratibu ambazo TBS tunafanya tuna huduma ambayo inaitwa Pre-Shipment Verification of Conformity (PVoC) ambapo kupitia utaratibu huo mteja anatakiwa akague bidhaa yake kule kwenye nchi ambako zinatoka.
Akikagua kule zinakotoka anapewa cheti kinachoitwa Certificate of Conformity (CoC) . Hiyo CoC ndiyo ataingia nayo nchini tutaihakiki ili kujua kama ni halisi, lakini pia tutakagua mzigo wake na baada ya hapo kama hautakuwa na shida yoyote ataruhusiwa kuuza mzigo wake nchini.''
Kwa upande wa mfanyabiashara ambaye atashindwa kuja na CoC, atatozwa faini ya asilimia 15 ya gharama za mzigo na baada ya hapo TBS itampimia mzigo (bidhaa)
''Bidhaa ikionekana ina shida itabidi airudishe nchi alikoitoa au ateketeze mzigo huo hapa nchini kwa gharama zake mwenyewe.''
Alifafanua kwamba kwa bidhaa nyingine za kawaida aambazo sio za chakula na vipodozi zitafuata taratibu za PVoC, lakini haina haja ya kuzisajili, kwa kuwa zinazosajiliwa ni za chakula na vipodozi.
Kuhusu wafanyabiashara waagizaji wa magari kutoka Japan, Haule alisema kwa sasa hivi shirika limebadilisha utaratibu mtu anatakiwa akague gari lake kutoka Japan, ambako shirika lina wakala wake wa ukaguzi wa magari.
''Kwa hiyo gari linatakiwa lije huku likiwa limeishakaguliwa kutoka Japan, mtu akija kutoka Japan hajakagua atatozwa faini na baadaye gari lake litakaguliwa hapa nchini.
Kwa wale wanaotoa magari nje ya Japan, Haule alisema magari yao yatakaguliwa hapa nchini kwa sababu bado kituo kwa ajili ya kazi hiyo, kipo.