AKAMATWA AKISAFIRISHA DAWA ZA KULEVYA MIRUNGI MAGUNIA 10 ARUSHA...ATUMIA UCHAWI KUKWEPA ASKARI

Na Abel Paul wa Jeshi la Polisi

Jeshi la Polisi mkoa wa Arusha limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja anayesafirisha madawa ya kulevya aina mirungi katika jiji la Arusha.


Akitoa taarifa hiyo leo Septemba Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishina wa msaidizi wa Polisi ACP Justine Masejo ameeleza kuwa tarehe 21.09.2022 muda wa saa 03:20 asubuhi huko maeneo ya Njiro katika Halmashauri ya Jiji la Arusha Jeshi hilo limefanikiwa kumkamata mtu mmoja aitwaye Benson Emmanuel (28) Mkazi wa Ngaramtoni, wilaya ya Arumeru akiwa anasafirisha madawa ya kulevya aina ya mirungi magunia 10 yenye uzito kilogramu 155.8.


Kamanda Masejo amebainisha kuwa Mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa anasafirisha madawa hayo ya kulevya kwa kutumia gari aina ya Toyota Rav 4 lenye namba za usajili T. 755 AWD huku akiwa amemwaga unga mweusi ambao unadhaniwa ni dawa za kienyeji kwa imani ya kutoonekana na vyombo vya ulinzi na usalama.


Aidha kamanda Masejo amewaambia waandishi wa Habari kuwa Uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa akijihusisha na mtandao wa usafirishaji wa madawa ya kulevya.


Pia Kamanda Masejo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi hilo kuhusiana na watu wachache wanaojihusisha na biashara haramu ya madawa ya kulevya ambayo yanaharibu vijana wengi na kupoteza nguvu kazi ya Taifa, hivyo akatoa onyo kwa baadhi ya watu wachache wanaojihusisha na biashara hiyo kuacha mara moja na kufanya biashara nyingine zilipo kisheria.

Sambamba na hilo ametoa wito kwa watu wachache wanaomiliki silaha kinyume na utaratibu wazisalimishe vituo vya Polisi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post