Muuguzi akionesha mojawapo ya njia salama za uzazi wa mpango ambayo ni kitanzi.
******************
Na Irene Mark
WAKATI Dunia ikiadhimisha siku ya uzazi wa mpango kila Septemba 26 ya mwaka, suala la utoaji mimba kwa njia zisizo salama linachangia ongezeko la vifo vitokanavyo na uzazi.
Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA), inaeleza kuwa vifo vya uzazi nchini Tanzania viliongezeka hadi vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015 kutoka vifo 454 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2010.
Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake na uzazi, Elias Kweyamba, anasema asilimia kati ya 16 hadi 19 ya vifo vya uzazi vinatokana na utoaji wa mimba usio salama.
Kwa sababu hiyo ipo haja ya Dunia husasani kwa nchi zinazoendelea kupata elimu sahihi ya njia za uzazi salama ili kuepuka mimba zisizotarajiwa ambazo mara nyingi hutolewa kwa njia hatarishi.
Wakizungumza na *HabariMseto Blog* kwa nyakati tofauti baadhi ya wanawake waliofika kwenye Zahanati ya Mpunguzi jijini Dodoma kupata huduma za kliniki pamoja na watoto wao wamesema elimu zaidi inahitajika hasa kwenye matumizi ya njia za uzazi wa mpango.
Wameeleza namna wanavyokosa elimu ya kupambana na maudhi madogomdogo baada ya kutumia njia za kupanga uzazi hali inayowalazimu kusitisha matumizi ya njia hizo na kuwasababishia kupata watoto wasiowatarajia ama kutoa mimba kwa njia hatarishi.
Wanawake hao pia hawana taarifa za uwepo wa siku ya kupanga uzazi duniani ambayo kimsingi inawahusu katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi lakini pia kuwa na afya njema huku wakishiriki kazi za kiuchumi kwa maslahi ya familia zao na taifa.
Katika kuadhimisha siku hiyo kila mwaka serikali, mashirika kibinafsi, vyombo vya habari na watu mbalimbali hukusanyika na kujadili masuala muhimu ya upatikanaji wa huduma bora za uzazi wa mpango.
Monica Agustino (22) kutoka Kijiji cha Mpunguzi ni mama wa watoto wanne, mkubwa ana miaka sita na mdogo ana miezi mitatu.
Anasema hivi sasa hata afya yake si nzuri kutokana na kupata watoto mfululizo huku akibainisha kwamba malezi ya watoto kwa kufanya vibarua kwenye mashamba ya watu ni magumu.
“Niliwahi kuzaa baada ya kukatisha masomo nikiwa kidato cha pili kijana niliyezaa naye ndio baba wa watoto wote hawa tunafurahi kuona watoto ila tunakabiliana na wakati mgumu katika malezi hasa wakiumwa.
“Nimesikia kuhusu njia za uzazi wa mpango nikiwa na mtoto wa pili nilitumia njia ya kijiti lakini nilishindwa kwa sababu waliniambia damu yangu haijaendana.
“Baada ya kuweka kijiti nikawa napata kizunguzungu, nakosa hamu ya kula, napata hedhi mfululizo na kuchoka sana ikabidi nikitoe sikumaliza muda mrefu nikabeba mimba ya mtoto wa tatu,” amesisitiza Monica.
Huku akitabasamu Monica anasema anatamani kupata njia ya uzazi wa mpango itakayomsaidia bila kupata maudhi yanayomuumiza mwili.
Anasema hakupata kwa wakati elimu ya uzazi wa mpango ndio maana amekuwa na familia kubwa inayomshinda kwenye malezi hivyo anakuwa tegemezi kwa ndugu na majirani.
“Kuna wakati tunakosa chakula na mimi ninanyonyesha basi napambana kuomba nikipata kidogo nawapa watoto mimi na baba yao tunavumilia.
Theresia Masanja (28) mwanakijiji kutoka Mpunguzi aliyekuwepo kwenye zahanati hiyo anasema mimba za mfululizo zilimfanya apoteze watoto wake wawili na kwamba baada ya kupata ushauri wa kitaalam wa njia za kisasa na bora za uzazi wa mpango amezifuata na sasa anaishi kwa furaha.
“Nilipata mimba nikiwa na mtoto wa siku 40 kwa huku kijijini kwatu ni aibu nikatafuta mbinu za kienyeji za kutoa mimba.
“Mtoto alikuwa na nyonya nikaelekezwa dawa nikanywa mimba ilishafikia miezi mitatu kumbe dawa ile niliyokunywa ni sumu kiumbe cha tumboni kilikufa na mimi hali yangu ikawa mbaya nilisafishwa kizazi huku nyumbani mwanangu mdogo aliugua na kwa kuwa hakunyonya hali ilikuwa mbaya akaletwa hospitali lakini haikuwa habati, mwanangu akafariki akiwa na miezi mitano.
“Nilipata elimu na vipimo nikakubaliana na watoa huduma na sasa natumia njia ya kitanzi. Nimebaki na watoto wawili mkubwa ana miaka 12 na mdogo ni huyu wa mwaka mmoja na nusu,” anasema Masanja huku akitabasamu.
Anazitaja njia nyingine za uzazi wa mpango anazozifahamu kuwa ni kondom, sindano, dawa, kijiti na kufunga uzazi.
Masanja alishauri elimu ya uzazi wa mpango iwafikie pia wanaume ili nao washiriki katika kutunza afya za wake zao na watoto.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Mussa Mfaume amesema ofisi yake imefungua milango kwa mashirika binafsi kupeleka elimu ya uzazi wa mpango kwa wanaume ambao ni wadau muhimu kwa mustakabali ya afya ya mwanamke na watoto.
“Licha ya kutoa kipaumbele kwa wanaume wanaokuja kliniki na wake zao kuoata huduma kwa haraka bado elimu zaidi inahitajika ili suala la afya ya uzazi liwe jambo la kifamilia,” amesisitiza Dk.Mfaume
Mtoa huduma wa afya ya uzazi na uzazi salama, Ozia Dominic, amesema wanawake wengi wanajitokeza kupata elimu kuliko wanaume hivyo wanawahamasisha kuwapeleka waume zao.
Hata hivyo tafiti mbalimbali za wataalam wa afya chini ya UNFPA zinaonesha kwamba zaidiee ya wanawake na wasichana bilioni 1.8 wako katika kundi la umri wa uzazi lakini wengi wao wanakabiliwa na vikwazo ambavyo ni ukosefu wa taarifa sahihi na huduma bora za kupanga uzazi kutoka kwa watumishi wenye utaalam.
Nchini Tanzania asilimia 32 tu ya wanawake walio katika umri wa uzazi wanatumia njia za kisasa za uzazi wa mpango huku asilimia 22 wakiwa na mahitaji ambayo hayajafikiwa.
Kwa kuzingatia kanuni zilizopo zinazowaweka wasichana kwenye ngono na ndoa za utotoni, asilimia 27 ya wasichana wenye umri kati ya miaka 19 na 15 ni wajawazito au wameanza kuzaa.
Matokeo yake, wanakabiliwa na hatari kubwa za kuharibika kwa mimba, utoaji mimba usio salama, aina nyingine za magonjwa ya uzazi ikiwemo saratani na vifo kutokana na matatizo ya ujauzito na uzazi.
Mbali na hayo, wanawake na wasichana wanashindwa kutimiza ndoto zao za maendeleo na kukabiliwa na kutengwa katika kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na vyombo vya maamuzi kwa sababu ya kushindwa kusimamia uzazi wao.
Huduma za kupanga uzazi ni moja ya afua mtambuka zinazopewa kipaumbele hasa katika huduma za kinga za afya.
Huduma hizo za ni muhimu katika kufikia malengo makuu ya afya hasa katika afya ya uzazi na mtoto. Inachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza vifo vya uzazi kwa takriban asilimia 44 kupunguza vifo vya watoto.
Huduma hizo ni muhimu katika ukuaji wa uchumi wa kaya na taifa, kuondoa umaskini na kupunguza njaa.
Pia zinasaidia kupambana na maradhi ya Upungufu wa Kinga Mwilini (UKIMWI), kukuza usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake, kuhakikisha uendelevu wa mazingira na kukuza uchumi wa mmoja mmoja na kaya kwa ujumla.
Social Plugin