Mwezesha kutoka OSHA, Dkt. Edwin Senguo, akiwasilisha mada kwa waajiri na viongozi wa matawi wa TUGHE waliohudhuria semina hiyo iliyofanyika jijini Mwanza Septemba 26 hadi 30, 2022.
Baadhi ya waajiri na viongozi wa TUGHE wa matawi mbali mbali nchini wakifuatilia mada zilizowasilishwa na OSHA katika semina ya waajiri na viongozi wa matawi wa TUGHE iliyofanyika jijini Mwanza kuanzia tarehe 26-30 Septemba, 2022.
Mwezesha kutoka OSHA, Dkt. Jerome Materu, akiwasilisha mada kwa waajiri na viongozi wa matawi wa TUGHE (hawapo pichani) waliohudhuria semina hiyo iliyofanyika jijini Mwanza.
***************************
Na Mwandishi Wetu
Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) umetoa mafunzo ya usalama na afya kwa waajiri na viongozi wa matawi ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) wapatao 800 nchi nzima ikiwa ni utekelezaji wa jukumu lake la msingi la kuongeza uelewa wa masuala husika miongoni mwa Watanzania wote.
Majukumu mengine ya OSHA ikiwa ni Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu- Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu ni pamoja na; kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003, kufanya tafiti mbali mbali zinazohusiana na masuala ya usalama na afya pamoja na kuishauri serikali kuhusiana na uundaji wa sera katika eneo husika.
Majukumu haya yote yamekuwa yakitekelezwa kwa minajili ya kulinda nguvukazi ya nchi na hivyo kuwezesha shughuli mbali mbali za kiuchumi kufanyika katika hali na mazingira salama.
Mafunzo hayo ya OSHA yametolewa kama sehemu ya mada zilizowasilishwa katika semina hiyo ya kitaifa iliyoandaliwa na TUGHE kwa waajiri na viongozi wa TUGHE toka katika maeneo mbali mbali ya kazi nchini.
Katika semina hiyo, OSHA iliwasilisha mada mbili; moja ikijikita kuelezea Sheria ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya mwaka 2003 pamoja na dhana nzima ya usalama na afya mahali pa kazi. Mada hii imewasilishwa na Dkt. Jerome Materu, ambaye ni Meneja wa Afya wa OSHA.
Aidha, mada nyingine imewasilishwa na Dkt. Edwin Senguo, Mkaguzi wa Afya kutoka OSHA ambaye alieleza zaidi kuhusu dhana nzima ya magonjwa yatokanayo na kazi na jitihada zinazochukuliwa na OSHA katika kudhibiti magonjwa hayo ikiwemo kuhakikisha kwamba wafanyakazi wanafanyiwa uchunguzi wa afya zao wanapoajiriwa, wakiwa kazini na pale wanapohitimishi muda wao wa ajira.
Akizungumza mara baada ya kuhitimisha mafunzo hayo, Dkt. Materu, ametoa wito kwa waajiri wote nchini kutumia vyema fursa ya mafunzo na ushauri wa kitaalam utolewao na OSHA ili kuboresha mifumo ya usalama na afya katika maeneo ya kazi.
“Kimsingi OSHA tumeendelea kutoa elimu ya usalama na afya mahali pa kazi ili kuwawezesha wadau wetu kutekeleza ipasavyo Sheria ya Usalama na Afya mahali pa kazi pamoja na miongozo mbali mbali inayotolewa kwa lengo la kuboresha mazingira ya kazi na hivyo kuleta tija katika uzalishaji. Niwaombe sana waajiri kutumia vizuri hizi fursa za mafunzo tunayoyatoa ili yaweze kuwasaidia katika kujenga mifumo imara ya usalama na afya katika maeneo yao ya kazi,” amesema Dkt. Materu.
Kwa upande wake Afisa Elimu wa TUGHE, Nsubisi Mwasandende amesema: “Mimi na washiriki wenzangu wa semina hii tumepata bahati ya kupokea mafunzo haya ya usalama na afya ambapo tumejifunza mambo mengi sana ikiwemo nini maana ya usalama kazini, masharti yakuzingatia ili kuhakikisha kwamba mahali pa kazi panakuwa salama, Sheria ya afya na usalama mahali pa kazi, umuhimu wa kamati za afya na usalama mahali pa kazi pamoja na vihatarishi na changamoto mbali mbali za usalama na afya na jinsi ya kukabiliana nazo. Hivyo, tunawashukuru sana watalaam wa OSHA kwa mafunzo mazuri. Aidha, tunawaomba OSHA waongeze nguvu zaidi katika ukaguzi kwenye maeneo ya kazi pamoja na kutoa ushauri kwa waajiri.”
“Nimefurahia sana mafunzo ya OSHA kwa siku ya leo, mada zote walizoziwasilisha zitakuwa na manufaa sana kwetu sisi kama watumishi na kwa waajiri pia katika kuboresha mazingira yetu ya kazi. Mathalani suala la kuwa na samani zinazokidhi vigezo vya usalama na afya limenivutia sana. Kwakweli mafunzo haya ni mazuri lakini kutokana na ufinyu wa muda ni vema wakatutembelea mara kwa mara katika maeneo yetu ya kazi na kutupatia elimu hii,” ameeleza Jackline Joseph Ngowi ambaye ni mtumishi wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Morogoro.
Social Plugin