*TCRA yashauriwa kuanzisha tuzo za wazalishaji maudhui bora
Na Mwandishi Wetu
Waandaaji wa Maudhui ya ndani yakiwemo maudhui ya burudani, elimu, Habari, Sanaa na michezo wamekumbushwa kuwa uwepo na ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ni fursa muhimu itakayowezesha kukuza sanaa na hatimae kukuza tija na kudumisha utamaduni unaojenga jamii imara.
Akizungumza wakati akifungua Warsha iliyowakutanisha Wadau wa Uzalishaji wa Maudhui ya Ndani wakiwemo Vituo vya Utangazaji, Waandaaji na Wasambazaji wa maudhui, wanazuoni wanaopika watayarishaji maudhui na waandaaji wa maudhuio ya kwenye mtandao Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Nape Moses Nnauye (Mb.) alisisitiza kuwa uwepo wa teknolojia mpya ya habari unawezesha wazalishaji maudhui kuifikia hadhira kubwa zaidi.Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb.) akiongoza kikao na Kamati ya Maudhui ya TCRA muda mfupi baada ya kufungua Warsha ya Waandaaji na Watayarishaji wa Maudhui iliyofanyika kwa siku mbili jijini Dar es salaam, ikiratibiwa na TCRA. Picha na: TCRA
“Ni ukweli usiopingika kwamba sasa mabadiliko ya teknolojia ya Habari na Utangazaji yametupeleka kwenye dunia nyingine ambayo usambazaji wa maudhui hauna mipaka. Kwa sasa unaweza kupokea maudhui kutoka sehemu yoyote duniani ili mradi unakifaa stahiki cha kupokelea maudhui. Makampuni makubwa ya kimataifa yanashindana kutengeneza na kusambaza Tamithiliya, Cartoon za Watoto, vichekesho (Comedy), Miziki, Makala na maudhui mengi yenye vionjo na tamaduni kutoka nchi mbalimbali. Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa tunatumia teknolojia iliyopo kuhakikisha kuwa na sisi tunaingia kwenye ulimwengu wa ushindani na utandawazi ambapo utavutia Watanzania na wananchi wengine walioko nje ya mipaka ya nchi yetu ili nao waweze kutazama na kueneza Utamaduni wetu na vilevile kuongeza pato la taifa,” alisisitiza Waziri Nape.
Alibainisha kuwa jamii imekumbwa na changamoto ya kulishwa maudhui kutoka nchi za mbali ambayo kwa kiasi kikubwa hayazingatii maadili na utamaduni wa Mtanzania na hivyo yamechangia sana kuharibu utamaduni wa ndani.
“Kila Jamii inayo maadili yake tofauti na jamii nyingine. Sisi kama jamii ya Watanzania tunao utamaduni wetu, mila na desturi ambazo zinatutofautisha na jamii nyingine za kigeni. Waandaaji na watayarishaji wa maudhui mnayo dhamana kubwa ya kuhakikisha kwamba utamaduni wetu,mila na desturi zetu zinadumishwa na hazipotoshwi kabisa ili hata watoto wetu wanaozaliwa kizazi hadi kizazi wawe na cha kujivunia katika nchi yao kupitia vipindi ama habari wanazozipata kupitia vyombo vya Habari na utangazaji,” aliongeza.
Akizungumzia lengo la kuandaa Warsha hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dkt. Jabiri Bakari alibainisha kuwa, Mamlaka hiyo imeamua kuwaleta pamoja wadau hao kwa kuzingatia kuwa wanayo nafasi kubwa ya kuiwezesha nchi kupata maudhui ya ndani yanayokidhi ubora.
“Kwa kuelewa umuhimu wa maudhui ya ndani TCRA imeamua kuratibu warsha hii ya siku mbili ili kujadili mustakabali mwema wa uzalishaji wa maudhui ya ndani yenye ubora,” aliongeza Mkurugenzi Mkuu wa TCRA.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo Dkt. Hassan Abbas akifunga warsha hiyo ya siku mbili alisisitiza kuwa Wizara hiyo itahakikisha inashirikiana na wadau wote wa maudhui kuhakikisha maudhui ya ndani yanapatikana kwa wingi ili kuviwezesha vituo vya utangazaji na usambazaji wa maudhui kufikisha maudhui ya ndani yenye kuisaidia nchi.
Miongoni mwa taasisi zilizowakilishwa kwenye Warsha hiyo ni pamoja na TASUBA, BASATA, Chuo Kikuu cha Dar es salaam-Shule ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma, Chuo Kikuu cha Dodoma(UDOM), Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari(WHMTH), Wazalishaji wa maudhui ya mtandaoni, Wakusanyaji na Wasambazaji wa maudhui, Watayarishaji binafsi wa maudhui, Vyombo vya Utangazaji, Waandishi wa Habari miongoni mwa makundi mengine yaliyoshiriki Warsha hiyo, iliyoazimia kwamba kila upande uwajibike, huku TCRA ikitolewa mwito na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mheshimiwa Nape Nnauye, kutafakari uwezekano wa kuanzisha tuzo maalum kwa wazalishaji bora wa maudhui ya ndani.
Social Plugin