***************************
*Waendeshaji wa Makundi ya Whatsapp watadharishwa kupokea maudhui na kuyaacha.
Na Mwandishi Wetu
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye ametoa onyo kali kwa wanaosambaza maudhui yanayohamasisha Mapenzi ya jinsia moja (ushoga na usagaji) kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuacha mara moja la sivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
Nape ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa Habari, amesema kuwa baadhi ya watumiaji wa maudhui ya kulipia mtandaoni wamekuwa wakichukua maudhui yenye viashiria vya mahusiano ya jinsia moja kisha kuyasambaza kwenye mitandao kwa madai ya kutoa elimu ya madhara yake huku wakisambaza na maudhui hayo.
"Tutawazoa watu kwa kutafuta mnyororo wote waliohusika katika usambazaji pamoja na Maadmin wa makundi hii itakuwa mfano na kujua serikali ipo" amesema Nape
“Ili kukomesha jambo hili Serikali imeonya kuwa yeyote atakaebainika kusambaza maudhui ya aina hiyo kwenye mitandao hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na viongozi wa makundi ya Makundi (Whatsaap Admin) na yeyote atakayetumiwa maudhui hayo usalama wake ni kuifuta na sio kuisambaza”Amesema Waziri Nape.
Aidha amesema kwa lengo la kuilinda jamii dhidi ya maudhui yasiyofaa Serikali imetoa angalizo na tahadhari na kutoa onyo kwamba wanaosambaza maudhui yanayochochea mahusiano ya jinsia moja watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
Waziri Nape amesisitiza kuwa siku za karibuni, kumekuwa na matukio mengi ya taarifa zinazosambazwa na baadhi ya watumiaji wa mitandao ya Kijamii ikionyesha video fupi zenye viashiria vya ushoga na kuleta taharuki kubwa miongoni mwa jamii kibaya zaidi wanatumia mgongo wa kuelimisha jamii.
Ameongeza kuwa, si kweli kwamba vyombo vya utangazaji nchini vimekuwa vikirusha maudhui ya mapenzi ya jinsia moja al’maarufu “ushoga” na kwamba baadhi ya watumiaji wa maudhui ya utangazaji wamekuwa wakinunua maudhui hayo kwa hiari yao kisha kukata vipande vifupi na kuvituma kwenye mitandao wakidai kuwa vituo vya utangazaji vinarusha aina hiyo ya maudhui.
“Napenda kusisitiza kuwa TCRA wamekuwa wakifuatilia na wamebaini kuwa hakuna kituo cha utangazaji kinachorusha maudhui yenye viashiria vya mapenzi ya jinsia moja,” alionya Nape.
Ameonya kuwa hata kama nia ya anaesambaza maudhui ya aina hiyo ni kutoa tahadhari, bado hatua zitachukuliwa kwa kuwa lengo la Serikali ni kukomesha kabisa usambazaji wa maudhui ya aina hiyo kwa kuwa yanachochea vitendo vya ushoga.
“Baadhi ya clips hizo zinatuhumu kwamba maudhui hayo yanarushwa na baadhi ya vyombo vya Utangazaji hapa Tanzania baada ya ufuatiliaji wa karibu kuhusu clips hizo zilizokuwa zinasambazwa, tumejidhihirisha kuwa kwa kupitia utandawazi wa maudhui duniani, baadhi ya watazamaji wa maudhui ya kulipia mtandaoni wamekuwa wakitazama aina ya maudhui hayo na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii” amesisitiza Nnauye.
Waziri alionya kuwa Serikali haitamuonea muhali mtu yeyote atakaehusika na kusambaza maudhui yenye viashiria vya ushoga.
“Nichukue nafasi hii kutoa onyo kwa yeyote atakayesambaza maudhui ya aina hiyo kwa jamii. Hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayehusika,” alisisitiza Waziri na kuongeza.
“Niendelee kusisitiza kuwa wajibu wa kuwalinda Watoto kutokana na maudhui yasiyofaa hasa kwenye mitandao ya kijamii ni wa kwetu sote ikianzia kwa Wazazi, Walezi na Mashuleni ambapo Watoto wetu hutumia muda mwingi huko wakiwa masomoni,” ameonya Waziri Nape.
Hata hivyo ameipongeza Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kazi nzuri ya kusimamia maudhui nchini; na kuongeza kuwa ni wakati sahihi kwa wananchi wote kulinda maadili ya nchi.
“Serikali kwa kutumia vyombo vyake, itaendelea kufuatilia kwa karibu wasambazaji wa maudhui yasiyozingatia maadili ya mtanzania ikiwa ni pamoja na yale yenye viashiria vya ushoga,” ameongeza.
Sambamba na hayo Waziri Nape ametoa wito kwa wazazi, walezi na walimu kuhakikisha kuwa wanawalinda watoto wao na utandawazi ambao ukitumiwa vibaya madhara yake ni mabaya kwa jamii na Taifa.
Social Plugin