Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ZAMA MPYA YAPIGWA FAINI YA MILIONI MBILI

Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Habbi Gunze akisoma hukumu dhidi ya Kituo cha Luninga Mtandaoni cha Zama Mpya baada ya kukiuka kanuni za maudhui ya Utangazaji, Jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Habbi Gunze akiwakabidhi hati ya hukumu Kituo cha Luninga Mtandaoni cha Zama Mpya baada ya kukiuka kanuni za maudhui ya Utangazaji, Jijini Dar es Salaam.

*************************

Na Mwandishi Wetu

KAMATI ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeitoza faini ya Shilingi milioni mbili luninga ya mtandaoni ya Zama Mpya kwa kosa la kuchapisha habari kuhusu tozo za serikali bila kuzingatia maadili hivyo kuhatarisha amani na usalama wa nchi.

Faini hiyo inatokana na kituo hicho kufanya mahojiano na Msanii Seleman Msingi 'Afande Sele' ambaye alikuwa akizungumzia masuala ya tozo bila kituo hicho kuzingatia maudhui ya utangazaji na maadili ya uandishi wa habari ya kuweka mizania ya habari.

Aidha, kituo hicho kimepewa onyo na kuwekwa chini ya uangalizi wa TCRA kwa miezi mitatu ili kuboresha utendaji kazi wao wa maudhui ya utangazaji

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Habi Gunze alisema Agosti 12, mwaka huu TCRA ilitoa leseni kwa Zama Mpya Tv na Agosti 28 mwaka huu walichapisha taarifa za uchochezi kuhusu tozo za serikali kwenye ukurasa wa twitter kinyume na kanuni ya 9 (a), 12 (a) (I) na 16 (1) aya 3 (a), (d), (g), (h) na (k) ya kanuni za kielektroniki na Posta ya mwaka 2020.

Alisema katika utetezi wa kituo hicho walikili kuchapisha habari hiyo huku wakieleza kiwa walitafuta na kuchapisha habari hizo kulingana na katiba na kwamba hawajui kilichochochewa na madhara yaliyopatikana.

"Kituo hiki kimetenda kosa la uchochezi kwa kuchapisha maudhui basi yanayohusu tozo za serikali kwa kutuhumu viongozi bila kutoa nafasi ya kujibu hivyo walikosa midhania. Pia taarifa yao haikuzingatia maadili na kanuni kwani imesababisha kuhatarisha amani, umoja na usalama wa nchi," alisema Gunze.

Aliongeza kuwa TCRA ina mamlaka ya kulinda maslahi ya serikali na watumiaji wa mitandao hivyo, wana mamlaka ya kufuatilia kila taarifa inayochapishwa.

Alisema kituo hicho kimekosa umakini katika usimamizi wa maudhui kwa sababu taarifa kutoka kwa mtu mmoja yenye kuilenga serikali haipaswi kuchapishwa bila kufuatilia na upande wa serikali.

"Kwa kuzingatia kanuni ya 21 (3) kamati inatoa adhabu ya faini ya Shilingi milioni mbili ambazo zinatakiwa kulipwa ndani ya siku 21 baada ya kusomwa hukumu hii, tunatoa onyo kali na tutaweka chini ya uangalizi kwa kipindi cha miezi mitatu ili kuhakikisha mnaboresha utendaji kazi wenu na haki ya kukata rufaa ipo wazi," alisisitiza Gunze.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com