Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BENKI YA CRDB YATWAA TUZO YA "BENKI BORA TANZANIA" KUTOKA JARIDA LA GLOBAL FINANCE

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (kulia) akipokea cheti cha tuzo ya "Benki Bora Tanzania" kutoka kwa Mwanzili na Mhariri Mtendaji wa Global Finance, Joseph Giarraputo, katika hafla ya kukabidhi tuzo kwa Benki Bora Duniani iliyofanyika kwenye ukumbi wa ‘National Press Club’, Washington, nchini Marekeni, Oktoba 15, 2022. Hii ni mara ya nne mfulululizo kwa Benki ya CRDB kutunikiwa tuzo ya Benki Bora nchini na jarida hilo maarufu duniani la biashara na fedha.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (watatu kushoto), na Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki hiyo, Tully Esther Mwambapa wakionyesha cheti cha tuzo ya "Benki Bora Tanzania" walichokabidhiwa na Mwanzili na Mhariri Mtendaji wa Global Finance, Joseph Giarraputo (wapili kushoto) katika hafla ya kukabidhi tuzo kwa Benki Bora Duniani iliyofanyika kwenye ukumbi wa The National Press Club, Washington, nchini Marekeni, Oktoba 15, 2022. Wengine pichani ni Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Mali, Joseph Maji (wapili kulia), Meneja Mwanadamizi wa Programu Endelevu, Kenneth Kasigila (wakwanza kulia), na Masele Msita, Meneja Biashara na Mahusiano ya Kimkakati.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akifuatia utoaji wa tuzo kwa Benki Bora Duniani uliyofanyika kwenye ukumbi wa The National Press Club, Washington, nchini Marekeni, Oktoba 15, 2022, ambapo kwa mara ya nne mfulululizo sasa Benki ya CRDB imekuwa ikitunikiwa tuzo ya Benki Bora nchini na jarida hilo maarufu duniani la biashara na fedha.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa (kakatiki) akiwa pamoja na Meneja Biashara na Mahusiano ya Kimkakati wa Benki hiyo, Masele Msita wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo kwa Benki Bora Duniani uliyofanyika kwenye ukumbi wa The National Press Club, Washington, nchini Marekeni, Oktoba 15, 2022, ambapo kwa mara ya nne mfulululizo sasa Benki ya CRDB imekuwa ikitunikiwa tuzo ya Benki Bora nchini na jarida hilo maarufu duniani la biashara na fedha.


========== ======== =========


Washington DC, Marekani - Benki ya CRDB imetunikiwa tuzo ya Benki Bora ya Tanzania kwa mwaka wa nne mfululizo, ikidhihirisha namna ambavyo benki hiyo imekuwa kiongozi katika huduma bora na utendaji sekta ya fedha nchini. Tuzo hiyo imetolewa na jarida maarufu duniani la biashara na fedha la Global Finance lenye makao yake mjini New York, Marekani.

Benki ya CRDB ilikabidhiwa tuzo hiyo wakati wa hafla ya chakula cha jioni iliyofanyika katika Klabu ya Kitaifa ya Waandishi wa Habari, Washighton, Marekani ambayo ilihudhuriwa na viongozi zaidi ya 900 wa sekta ya fedha kutoka kote ulimwenguni.

Tuzo hiyo inatambua ukuaji endelevu wa Benki ya CRDB, ambao umekuwa ukinufaisha wateja, wawekezaji na uchumi wa nchi kwa ujumla. Tuzo hiyo pia inatambua mafanikio ya mkakati wa benki hiyo wa mabadiliko ya kidijitali, ambao umechochea ubunifu wa huduma za kidijitali hivyo kuongeza ujumuishaji wa kifedha nchini.

"Tunajivunia kutambuliwa kama Benki Bora ya Tanzania na Global Finance kwa mara nyingine tena. Hii inaonyesha kwamba tuko kwenye njia sahihi ya kutoa huduma bora kwa wateja wetu na kujenga thamani kwa wanahisa wetu sambamba na kuleta mabadiliko katika sekta ya fedha nchini," alisema Abdulmajid Nsekela, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB.

Kwa miaka minne iliyopita, Benki ya CRDB imekuwa ikiboresha mifumo yake ya utoaji huduma ili kuwapa wateja huduma za kiwango cha kimataifa. Benki hiyo pia imekuwa ikupanua wigo wa bidhaa zake, na kuimarisha mtandao wake kwa kuwekeza kwenye njia za kidijitali za utoaji huduma.

Nsekela aliwashukuru wateja, wanahisa na wawekezaji wa Benki hiyo kwa mafanikio ya tuzo hiyo. Kwa sasa Benki ya CRDB ndiyo benki kubwa zaidi nchini Tanzania, ikiwa na mali ya zaidi ya TZS 10 Trilioni. Benki pia inaongoza kwa amana za wateja (Shilingi Trilioni 7) na mikopo ya awali (Shilingi Trilioni 6).

Jopo la majaji wa tuzo za Global Finance limeichagua Benki ya CRDB mahususi kwa ajili ya mafanikio yake katika viashiria vyote vya biashara. “Katika kipindi cha mwaka jana, tumeshuhudia Benki ya CRDB ikifanya maboresho makubwa katika huduma kwa wateja, hususan huduma za kidijitali,” alisema Joseph Giarraputo, Mwanzilishi na Mhariri Mtendaji wa Global Finance.

Giarraputo pia alitaja kuwa tuzo hiyo inatambua kazi ya kupongezwa iliyofanywa na Benki ya CRDB katika kusaidia sekta za biashara na wajasiriamali wadogo na wa kati katika kuondokana na changamoto zilizosababishwa na janga la UVIKO-19. "Juhudi zote hizi zimeendelea kuimarisha benki hii, na kupelekea utendaji mzuri," aliongeza.

Benki ya CRDB imeendelea kupata matokeo mazuri ya kifedha mwaka hadi mwaka, katika mwaka wa fedha uliopita ilipata faida ya Shilingi bilioni 268.2, sawa na ongezeko la asilimia 62.3 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 165.2 mwaka 2020. Katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka 2022, ilipata faida Shilingi bilioni 174 bilioni, kulinganisha na Shilingi bilioni 88 katika kipindi kama hicho mwaka jana.

Nsekela amesema matokeo mazuri ya kifedha ya Benki ya CRDB kwa kiasi kikubwa yanachangaiwa na mazingira mazuri ya biashara nchini. Aliishukuru Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji.

Hii ni tuzo ya pili ya Benki ya CRDB ya 'Benki Bora Tanzania' mwaka huu, kufuatia tuzo kama hiyo kutoka kwa jarida maarufu la fedha na uchumi la Uingereza la Euromoney mwezi Julai.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com