Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHIRIKA LA DSIK TANZANIA LAKABIDHI MAHITAJI YA SHULE KWA WANAFUNZI JIJINI MWANZA


Shirika linalojihusisha na utoaji elimu ya fedha nchini, DSIK Tanzania limekabidhi mahitaji mbalimbali ikiwemo mabegi, madaftari (Counter Books), kalamu na taulo za kike katika Shule ya Sekondari Nyakurunduma jijini Mwanza.


Akizungumza wakati wa zoezi la kukabidhi mahitaji hayo lililofanyika Oktoba 27, 2022, Mkurugenzi Mkazi wa shirika hilo Stephen Safe alisema hatua hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Akiba Duniani ambayo huadhimishwa wiki ya mwisho ya mwezi Oktoba kila mwaka.


Alisema mahitaji hayo yatawasaidia wanafunzi 80 ambao ni wanachama wa Klabu ya Akiba iliyoanzishwa na shirika la DSIK Tanzania katika Shule ya Sekondari Nyakurunduma ili kujifunza kwa ufasaha elimu ya fedha hukU tauro/pads zikiwasaidia wanafunzi wa kike kutokosa masomo wakati wa hedhi.


Safe aliwahimiza wanafunzi kuwa na mtazamo chanya kuhusu masuala ya fedha, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kujiwekea malengo na kutunza akiba ili kutimiza malengo hayo akisema "weka akiba leo ili kesho yako iwe imara"


Naye Mkufunzi wa Elimu ya Fedha Shirika la DSIK Tanzania, Rukia Amin alisema shirika hilo linatoa elimu ya fedha kupitia Klabu za Akiba katika Shule za Msingi na Sekondari zipatazo 90 jijini Mwanza ili kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya fedha hususani kuweka akiba wangali bado wadogo ambapo kwa mwaka 2021/22 zaidi ya wanafunzi elfu saba wamenufaika na elimu hiyo.


Kwa upande wao baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyakurunduma akiwemo Petro Leston na Mariam Zacharia walisema Klabu ya Akiba imewajengea uelewa kuhusu masuala ya kifedha hususani utaratibu wa kutunza akiba kupitia fedha za matumizi wanazopewa na wazazi na pia kuanzisha shughuli za ujasiriamali ikiwemo ufugaji wa kuku na sungura wangali bado shuleni hatua itakayowajenga kwa maisha ya baadae.


"Klabu ya Akiba imetuwezesha kutunza akiba tofauti na hapo awali ambapo tulikuwa tukipewa hela ya matumizi ya shule tunatumia yote. Tunawashukuru sana DSIK Tanzania kwa kutupatia elimu ya fedha na pia mahitaji ya shule ikiwemo mabegi na madaftari, hatutawaangusha kwani tutasoma kwa bidhii ili tutimize malengo yetu" alisema Glory Ehad na Samwel Mihayo.
Na George Binagi-GB Pazzo, BMG
Mkurugenzi Mkazi wa shirika la DSIK Tanzania, Stephen Safe (kushoto) akikabidhi mahitaji ya shule ikiwemo mabegi, madaftari, kalamu pamoja na taulo za kike kwa wanafunzi wanaoshiriki Klabu ya Akiba katika Shule ya Sekondari Nyakurunduma jijini Mwanza.
Mkurugenzi Mkazi wa shirika la DSIK Tanzania, Stephen Safe akizungumza kwenye zoezi fupi la kukabidhi mahitaji mbalimbali kwa wanafunzi wanaoshiriki Klabu ya Akiba katika Shule ya Sekondari Nyakurunduma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Akiba Duniani 2022.
Mkurugenzi Mkazi wa shirika la DSIK Tanzania, Stephen Safe akizungumza wakati wa zoezi hilo.
Mkufunzi wa Elimu ya Fedha kutoka Shirika la DSIK Tanzania, Rukia Amin akizungumza wakati wa zoezi la kukabidhi mahitaji ya shule kwa wanafunzi 80 wanaoshiriki Klabu ya Akiba katika Shule ya Sekondari Nyakurunduma jijini Mwanza.
Mwakilishi kutoka Shirika la DSIK Ujerumani, Fabian Partsch akitoa salamu zake.
Wanafunzi wanaoshiriki Klabu ya Akiba katika Shule ya Nyakurunduma wakifuatilia hafla hiyo.
Wanafunzi wa Nyakurunduma Sekondari jijini Mwanza.
Picha ya pamoja.
Picha ya pamoja.
Mwanachama Klabu ya Akiba Nyakurunduma Sekondari jijini Mwanza, Petro Leston akieleza umuhimu wa elimu ya akiba.
Mwanachama Klabu ya Akiba Nyakurunduma Sekondari jijini Mwanza, Mariam Zacharia akieleza mahitaji yaliyotolewa na shirika la DSIK Tanzania yatakavyowasaidia kujifunza.
Mwanachama Klabu ya Akiba Nyakurunduma Sekondari jijini Mwanza, Samwel Mihayo akizungumzia umuhimu wa elimu ya fedha kwa wanafunzi mashuleni.
Mwanachama Klabu ya Akiba Nyakurunduma Sekondari jijini Mwanza, Glory Ehad akitoa shukurani kwa shirika la DSIK Tanzania kwa kuwasaidia mahitaji ya shule.
Mwalimu Fatina Kayela wa Shule ya Sekondari Nyakurunduma jijini Mwanza ambaye pia ni Mwalimu wa Klabu ya Akiba shuleni hapo alisema Klabu hiyo imetoa ari kwa wanafunzi kujifunza elimu ya fedha.
Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Nyakurunduma jijini Mwanza wakiwa na vifaa mbalimbali vya shule ikiwemo mabegi waliyokabidhiwa na shirika la DSIK Tanzania.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com