Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe.Sophia Mjema akisaini moja ya Mkataba wa Lishe kabla ya kuukabidhi kwa wakuu wa wilaya.
Na Michael Utouh- Shinyanga
Mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mh. Sophia Mjema amewaasa Viongozi wote kuanzia wakuu wa wilaya,wakurugenzi,makatibu tawala wakuu wa idara, ngazi zote za wilaya,kata hadi kijiji kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha maagizo yote yanayotolewa toka ngazi za juu yanatekelezwa kwa haraka na wasiwe kikwazo katika kufelisha jitihada zozote za kimaendeleo.
Ametoa maelekezo hayo wakati wa ufunguzi wa kikao Cha Kamati ya huduma za afya ya msingi Mkoa wa Shinyanga kuhusu kupambana na ugonjwa wa ebola sambamba na kusaini mkataba wa utekelezaji wa afua za lishe.
Katika kikao hicho Mhe. Mjema amewaeleza wajumbe wote waliofika katika kikao hicho kuwa kila mjumbe ana wajibu wa kutoa elimu kwa wananchi wote kuhusu umuhimu wa kufahamu njia muhimu za kujihami na ugonjwa huo kwa wakati huu ambao bado hakuna maambukizi yeyote ndani ya nchi
Ameongeza endapo wananchi watapewa elimu nzuri ya kufahamu umuhimu wa kukabiliana na Ebola pamoja na dalili zake itasaidia kupunguza kasi kubwa ya maambukizi kama kukitokea mlipuko wa ugonjwa huo kwani kulingana na maelekezo ya wizara ya afya yanautaka kila mkoa kuweka nguvu kubwa katika kutoa elimu,kufanya maandalizi ya awali endapo kukiripotiwa mlipuko wa mgonjwa yeyote wa ebola
Akitaja vituo ambavyo mkoa umeviandaa endapo kukiripotiwa mgonjwa yeyote ndani ya Mkoa amesema kuwa vituo hivyo ni pamoja na Hospitali ya rufaa ya mwawaza jengo la dharura kwa Manispaa ya Shinyanga, Kituo cha afya kishapu kwa halmashauri ya kishapu, Kituo cha afya Nyasubi kwa Manispaa ya kahama, Hospital ya ushetu jengo la dharura kwa halmashauri ya ushetu, Kituo Cha Afya Bugarama kwa halmashauri ya msalala, pamoja na Hospital ya wilaya Shinyanga kwa halmashauri ya Shinyanga.
"Ndugu wajumbe naomba nitoe wito kwenu kupitia kikao hiki kwenda kuhamasisha jamii kutekeleza maagizo yanayotolewa na wizara ya afya kupitia wataalamu wa afya kuhusu kujikinga na ugonjwa wa Ebola ikiwemo kuendelea kunawa mikono kwa maji safi tiririka na sabuni, kutumia vitakasa mikono(Sanitizer) kutokushikana mikono na kukumbatiana, kusafisha mazingira yote na kuwa na usafi binafsi wakati wote", amesema Mhe.Mjema.
Katika kikao hicho Mhe. Mjema ameweza kuzungumzia kuhusu utekelezaji wa afua za lishe huku akisema kuwa mnamo tarehe 30/09/2022 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliingia makubaliano ya kutekeleza mkataba wa afua za lishe na Wakuu wa mikoa kote nchini.
Mkataba huo uliosainiwa utakuwa wa miaka nane(8) kuanzia Julai 2022 hadi Juni 2030 huku mkataba huo ukiwa na viashiria 14 na 12 vikiwepo kwenye mkataba uliokwisha muda wake huku viashiria viwili vikiongezeka, viashiria vilivyoongezeka ni pamoja na idadi ya shule zinazotoa chakula mashuleni kulingana na mwongozo na idadi ya wanafunzi ili kuweza kukabiliana na tatizo la lishe duni.
Akitolea msisitizo wa utekelezaji wa maagizo yote yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa wakuu wa mikoa,makatibu tawala kwenda kwa Viongozi wote ngazi ya wilaya hadi vijiji yanatekelezwa kwa haraka na sio kuwa na kusuasua kwani agizo lolote linalotolewa na Rais huwa ni amri katika kutekelezwa.
"Naomba niwaweke wazi kuwa sintomvumilia yeyote yule atakayekuwa kikwazo katika kukwamisha utekelezwaji wa majukumu yanayotolewa na Rais kwani tunapaswa kufahamu kuwa agizo lolote la Rais ni sawa na moto unapaswa kuogopa na kulitekeleza kwa haraka nataka mkoa wangu wa Shinyanga uwe kwanza kwa kila kitu hivyo sitaki kuwa na watumishi ambao watakuwa ni wa kwanza katika kukwamisha utekelezaji", amesema Mhe. Mjema
Baadhi ya wajumbe waliofika kwenye kikao hicho kilichofanyika kwenye ukumbi wa Mkuu wa Mkoa Shinyanga ( picha na John Ndaki)
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Prof. Siza D. Tumbo akizungumza wakati wa kikao.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe.Sophia Mjema, Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga Prof. Siza D. Tumbo wa kwanza kushoto wakisaini moja ya Mkataba wa Lishe kabla ya kuukabidhi kwa wakuu wa wilaya.
Social Plugin