Mkurugenzi Mtendaji wa TAMCODE, Rose Ngunangwa Mwalongo
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Shirika la Vyombo vya Habari kwa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TAMCODE) limetoa wito kwa Majaji kutoa hukumu ya kifungo cha maisha kwa washtakiwa wa mauaji badala ya kifo ili kuokoa watu wasiokuwa na hatia.
Akizungumza na Waandishi wa Habari, Mkurugenzi Mtendaji wa TAMCODE, Rose Ngunangwa Mwalongo Leo Oktoba 10 ikiwa ni Siku ya Kupinga Adhabu ya Kifo Duniani amesema TAMCODE inaungana na dunia kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupinga Adhabu ya Kifo ambapo kauli mbiu ya mwaka huu 2022 ni ‘Hukumu ya Kifo, Njia Iliyogubikwa na Utesaji.’
Mwalongo anaeleza kuwa Kauli mbiu hii inakuja wakati ambapo dunia imeshuhudia baadhi ya shuhuda juu ya waliohukumiwa kifo kuwa walikubali makosa kutokana na kushurutishwa kwa njia za utesaji.
“Iwe ni Kweli au la mchakato wa kuhojiwa unaweza kuwa na matatizo na ni vigumu sana kuthibitisha kama mtuhumiwa alitoa ushahidi kwa kushurutishwa au la. Itoshe tu kusema kuwa yapo mambo mengi ambayo yamejificha katika kila ushahidi uliotolewa”,amesema.
“TAMCODE inatambua uwepo wa Kifungu cha 197 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambacho kinaweka bayana kuwa ‘Mtu anayepatikana na kosa la mauaji atahukumiwa kifo,’ lakini pia inatambua kwamba kumekuwepo na majaji ambao wametoa hukumu mbadala badala ya kifo, ambapo wale ambao wangehukumiwa kunyongwa, walihukumiwa kifungo cha maisha”,ameeleza.
Amesema TAMCODE inatambua pia jitihada zote za Rais aliyepo madarakani Mhe. Samia Suluhu Hassan ambaye hajasaini hukumu ya kifo na nia njema ya kubatilisha adhabu za wale waliohukumiwa kifo, hali ambayo imeifanya Tanzania kuwa katika rekodi ya kutokunyonga tangu mwaka 1994. Hakika hili linastahili kupongezwa.
“Wakati tunapongeza nchi yetu kutokunyonga kwa muda mrefu, TAMCODE inapenda kuunga mkono wito uliotolewa na mmoja wa Majaji wastaafu wazoefu wa Mahakama ya Rufaa Tanzania Madam Engera Kileo juu ya haja ya kuondoa hukumu ya kifo katika sheria kutokana na aliyenyongwa kutokuwa na nafasi ya kubatilishiwa hukumu kwani “mahakama zinaweza kufanya makosa na upo uwezekano wa kufanya makosa ya kibinadamu ambayo yanaweza kusababisha watu wasiokuwa na hatia kunyongwa”,amesema Mwalongo.
Mwalongo amebainisha kuwa TAMCODE inapendekeza Majaji watumie utashi wao kutoa hukumu za kifungo cha maisha badala ya hukumu ya kifo kwani ni suala lisilofichika kuwa mahakama zinaweza kufanya makosa, hali ambayo inaweza kusababisha watu wasiokuwa na hatia kuhukumiwa kifo. Tuna imani kuwa hii itasaidia wale waliohukumiwa kimakosa kuwa na nafasi nyingine ya kukata rufaa na pengine kupewa msamaha.
“Pia Bunge lipitie upya na kufanyia marekebisho ya baadhi ya sheria ikiwa ni pamoja na Sheria ya Magereza ya mwaka 1967 na haswa vifungu ambavyo vinaweka vikwazo kwa waandishi wa habari kupata taarifa kutoka magerezani. Vifungu hivyo vitengeneze mazingira ya sera ya uwazi kama ilivyo kwa Kenya na Uganda”,amesema Mwalongo.
Amesema TAMCODE inapendekeza Bunge lifanyie marekebisho Kifungu cha 197 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kuwa na kifungo cha maisha badala ya hukumu ya kifo ili kutoa nafasi kwa majaji kutumia utashi wao wa kisheria kuamua vinginevyo kuliko ilivyo sasa ambapo majaji wengine wanahisi kuwa wamefungwa mikono.
“Mapendekezo mengine ni Wizara ya Afya itenge rasilimali zaidi kwa ajili ya afya ya akili kuwezesha kubaini dalili za awali za msongo wa mawazo na sonona ambavyo vinaweza kuwa sehemu ya sababu za baadhi ya mauaji yaliyojitokeza nchini katika miaka ya hivi karibuni na hivyo kupelekea watuhumiwa wengi kuhukumiwa kunyongwa”,ameongeza.
Mwalongo amesema TAMCODE ingependa kila mtu kujifunza kutokana na maneno ya Rob Warden, Mkurugenzi Mtendaji wa “Centre on Wrongful Convictions” (Kituo cha Hukumu za Kimakosa) ambapo alinukuliwa akisema “Iwe unaunga mkono au unapinga hukumu ya kifo, msimamo wako utabadilika pale utakaposoma maneno ya mwisho ya aliyehukumiwa kunyogwa—mengine ni ya huzuni, mengine yasiyofaa kusikia, mengine ya kuchekesha, yote ni janga. Kitu kinachotisha zaidi ni kufikiria kuwa baadhi ya wale walioshuhudia kuwa hawana hatia hadi mwisho huenda wanaweza kuwa walikuwa wanasema kweli.”
Amesema hofu waliyo nayo TAMCODE kuwa wengine ambao wameshuhudia kuwa hawana hatia hadi mwisho huenda ni kweli walikuwa hawana hatia.
Shirika la Vyombo vya Habari kwa Maendeleo ya Jamii Tanzania (TAMCODE)ni asasi isiyokuwa ya kiserikali inayojitoa kuchangia maendeleo ya jamii kupitia kujengea uwezo, kufanya tafiti na utetezi ili kuwezesha vyombo vya habari vya kitaifa na vya kijamii kutoa taarifa za masuala ya maendeleo kwa kuzingatia utu, huruma, kutokufungamana na upande wowote na kutumia jicho la jinsia.
Social Plugin