Baraka Mayala akiendelea kupata matibabu hospitalini
Na Halima Khoya - Shinyanga
Baraka Mayala (24) Mkazi wa Burugalila Kata ya Kizumbi Manispaa ya Shinyanga, amenusurika kifo kwa kucharangwa mapanga kichwani na sehemu mbalimbali za mwili wake na watu ambao hawakufahamika wakati akitoka kwenye harusi.
Tukio hilo limetokea Oktoba 7, mwaka huu majira ya saa 4 usiku.
Akisimulia tukio hilo leo Mayala amesema watu hao ambao hawafahamu waliokuwa zaidi ya 10 walimvamia njiani wakati akitoka kwenye harusi majira hayo ya saa 4 usiku na kuanza kumshambulia kwa kumkata mapanga kichwani na sehemu zingine na mwili wake na kisha kumpora kiasi cha fedha Sh. 10,000/= na simu ya mkononi.
"Watu hawa walinivamia njiani nikitoka kwenye harusi na kuanza kunikagua kwenye mifuko ya suruali na wakati nikijitetea ndipo wakaanza kunishambulia kwa mapanga na wamenikata kichwani mara mbili,na nilipotaka kukimbia walinikata katika miguu yangu, na nilipotaka kutambaa kwa mikono walinikata mikononi kisha wakachukua Sh. 10,000 na simu ya mkononi wakakimbia",amesema Mayala.
Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa mkoani Shinyanga Dk. Kambi Buteta, alithibitisha kumpokea kijana huyo hopitalini hapo na wanaendelea kumpatia matibabu.
"Tulimpokea Majeruhi kijana Baraka Mayala akiwa na majeraha kichwani, majeraha ambayo yanaashiria alijeruhiwa na kitu chenye ncha kali, lakini tulifanikiwa kumpatia huduma ya kwanza ili kuzuia damu zisiendelee kuvuja ambapo hali ya kijana huyo ni nzuri kiasi na bado anaendelea kupata matibabu zaidi",amesema Dk, Buteta.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Jackson Mwakagonda, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kubainisha kuwa Jeshi la polisi linaendelea na upelelezi.
Social Plugin