Na Mwandishi Wetu, Tabora
MKUU wa Mkoa wa Tabora Dk.Batilda Buriani ameipokea kwa mikono miwili Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao pamoja na Strong Women ambao wamefika kwenye mkoa huo kwa ajili ya Kampeni ya Samia Nivishe Viatu 2022.
Lengo kuu la Kampeni ya Samia Nivishe Viatu ni kwamba kila mtoto mwanafunzi mwenye uhitaji anavaa kiatu cha Samia Suluhu na kampeni hiyo itafanyika katika mikoa yote nchini kulingana na ratiba.
Akizungumza mbele ya Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao Steven Mengele maarufu Steve Nyerere pamoja na wawakilishi wa Stong Women, Dk.Batilda amesema kinachofanywa na taasisi hiyo kinadhihirisha sanaa ni kioo cha jamii.
“Ninyi mmeangalia kupitia kazi mnazofanya za sanaa mkajua changamoto zilizoko kwenye jamii na mkaguswa lakini mmeenda mbali zaidi kwa kuona jinsi gani mtamshika mkono Mama Samia ili awafikie watanzania wenye matatizo.
“Na mngeweza kupata viatu vya mtumba lakini mkasema mtanunua viatu vipya ili mtoto wa kijijini kabisa ajue jinsi gani Mama Samia alivyokuwa na mapenzi na Watanzania na mkasema basi mtapeleka viatu vipya.Niseme tu kwa jinsi ambavyo mmefanya Mwenyezi Mungu akawazidishe riziki pale mlipotoa , akawang’arishie nyota zenu katika kazi,”amesema Dk.Buriani.
Aidha amesema kinachofanywa na taasisi ya Mama Ongea na Mwanao pamoja na Strong Women ni funzo kubwa na wamefika Tabora kwenye mkoa wenye uhitaji mkubwa.
“Tunavyokwenda huko vijijini tunaona changamoto kubwa na tunasema tuone jinsi gani tutaweza kufanya mmoja mmoja lakini ninyi mmekuja kikundi, mkiwa na maono makubwa ya kusambaza viatu hivi Tanzania nzima, kwa hiyo mmeacha alama na tutatafuta wadau ili kuongeza nguvu kwenye hili mnalolifanya.
“Niseme tu tumefurahi sana, tumefarijika sana , tunashukuru na kwa hakika Mama Samia amewavisha watoto wa Tabora kupitia ninyi wenzetu wa Mama Ongea na Mwanao kwa kushirikiana na Strong Women na kweli mmeongea na wenetu hapa Tabora,”amesisitiza Dk.Buriani.
Awali Mwenyekiti wa Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao Steve Nyerere alimueleza Dk.Buriani wamefika kwenye mkoa huo na watakwenda vijijini kugawa viatu kwa wanafunzi wenye uhitaji.
“Kwasababu hatutaki kukabidhi kiatu kwa Mwalimu Mkuu kunakuwa na changamoto kidogo, hivyo sisi wenyewe ndio tunamvisha mtoto kiatu na anaondoka nacho.Viatu vyenyewe ni hivi hapa mfano wake(akaonesha) tukasema tuje tukuoneshe uvione ili tuendelee na kampeni yetu kwenye mkoa wako,
Kwa hiyo Mimi na Wenzangu baada ya kupata ridhaa yako Mkuu wa Mkoa tutaelekea katika Kata ya Ikongolo,Wilaya ya Uyui katika shule ya Msingi Ikongolo kuwapelekea Wanafunzi wenye uhitaji wa viatu vya Mama samia'' alisema Steve.
Wanafunzi wa Shule ya Msingi Ikongolo Kata ya Ikongolo,Wilaya ya Uyui wakifurahia viatu walivokabidhiwa na Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao na Strong Women.
MKUU wa Mkoa wa Tabora Dk.Batilda Buriani akizungumza wakati akiikaribisha Taasisi ya Mama Ongea na Mwanao chini ya Mwenyekiti wake Steven Mengere almaarufu Steve Nyerere wakiwa sambamba na Strong Women ambao walifika kwenye mkoa huo kwa ajili ya Kampeni ya kutekeleza kampeni yao ya 'Samia Nivishe Viatu2022'.Pichani kulia ni Mwenyekiti wa taasisi ya Mama Ongea na Mwanao Steven Mengere almaarufu Steve Nyerere
MKUU wa Mkoa wa Tabora Dk.Batilda Buriani akiwa ameambatana na Mwenyekiti wa taasisi ya Mama Ongea na Mwanao Steven Mengere almaarufu Steve Nyerere mara baada ya kuwasili ofisi za Mkuu wa Mkoa mkoani Tabora kwa ajili ya kutekeleza kampeni yao ya 'Samia Nivishe Viatu2022'.