Meneja wa Benki yaa CRDB Kanda ya Magharibi, Saidi Pamui akizungumza na waandishi wa habari leo Mjini Shinyanga
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Benki ya CRDB inatarajia kuadhimisha Kumbukizi ya Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Oktoba 14,2022 kwa kufanya Tamasha la Mbio za Baiskeli litakaloambatana na hamasa ya uchangiaji damu salama kwa ajili ya wahitaji wa damu katika hospitali ya Mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza na Vyombo vya Habari leo Jumatano Oktoba 12,2022, Meneja wa Benki yaa CRDB Kanda ya Magharibi, Saidi Pamui amesema Mashindano ya Baiskeli yameandaliwa Benki ya CRDB kupitia tawi la Shinyanga.
“Tamasha la Mbio za Baiskeli litapambwa na mashindano ya mbio za baiskeli zenye washiriki 275 wakataogawanyika katika makundi matatu. Kundi la kwanza ni la Wabobevu wa baiskeli watakaokimbia kilomita 150 (Shinyanga- Isaka) ambapo mshindi wa kwanza atapata zawadi ya pesa taslimu kiasi cha shilingi 1,500,000/=”,amesema Pamui.
“Pia kuna kundi la Vijana watakaozunguka uwanja wa CCM Kambarage Mjini Shinyanga mara 60 ambapo mshindi wa kwanza atapata zawadi ya shilingi 500,000/=, kundi la tatu ni la wanawake ambao watazunguka uwanja wa CCM Kambarage mara 40 ambapo mshindi wa kwanza atapata zawadi ya shilingi 500,000/=”,ameeleza Pamui.
Amefafanua zaidi kuwa katika Tamasha la Mbio za Baiskeli, Benki ya CRDB inakusudia kutoa shilingi 6,450,000/= zawadi kwa washindi 40 kwa viwango mbalimbali.
“Katika tamasha hili pia kutakuwa na bonanza la mpira wa miguu kati ya CRDB Digital FC na SHUWASA, ngoma naa nyimbo kutoka kwa wasanii mbalimbali na sanaa nyingine nyingi zikishuhudiwa na wananchi wa mkoa wa Shinyanga na mikoa jirani”,ameongeza Pamui.
“Tunakusudia kukusanya lita 500 za damu, kukutanisha watu zaidi ya 2000 wakiwemo wana michezo wa baiskeli 275. Tunategemea kuongeza mahusiano kati ya wafanyakazi wa Benki ya CRDB na Jamii ya Shinyanga. Pia Benki ya CRDB itatoa elimu ya huduma za Benki kwa jamii”,amesema Pamui.
“Karibuni sana katika Tamasha la Mbio za Baiskeli CRDB Shinyanga. Baba wa taifa alikuwa mdau wa baiskeli na mashindano ya baiskeli yanapendwa sana na wananchi. Napenda kuwafahamisha kuwa CRDB hatuna jambo dogo, tukutane uwanja wa CCM Kambarage Oktoba 14,2022. Mwaka huu jambo letu ni kubwa sana",amesema Pamui.
Amesema Benki ya CRDB imejiwekea utamaduni wa kutoa msaada kwa jamii ili kupambana na changamoto zinazozuia maendeleo ya jamii ikiwa ni mkakati wake wa kuwekeza katika jamii husika na kwa sehemu kubwa ya mkakati huo unajikita sana katika kutatua changamoto zilizopo kwenye sekta ya elimu, afya na michezo.
Meneja wa Benki yaa CRDB Kanda ya Magharibi, Saidi Pamui akizungumza na waandishi wa habari leo Mjini Shinyanga