Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BARAZA LA WAFANYAKAZI PURA LARIDHISHWA UTENDAJI KAZI WA TAASISI


Sehemu ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi PURA wakiwa katika kikao kilicholenga kujadili taarifa za utekelezaji wa Taasisi hiyo kwa mwaka 2021/22 na robo ya mwaka 2022/23. Kikao hicho kilifanyika Jijini Arusha hivi karibuni na kuongozwa na Mwenyekiti wa Baraza hilo, Mha. Charles Sangweni.Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi PURA katika picha ya pamoja mara baada ya kikao. Walioketi kutoka kulia ni Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam (Bi. Sara Rwezaula), Katibu wa TUGHE Tawi la PURA (Mha. Fabian Mwose), Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi PURA (Mha. Charles Sangweni), Katibu Msaidizi wa Baraza la Wafanyakazi PURA (Bw. Ebeneza Mollel) na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Taasisi PURA (Bw. Rogasian Ngumbi)

Sehemu ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi PURA wakifuatilia taarifa zilizokuwa zikiwasilishwa katika kikao hicho

Mjumbe wa Baraza kutoka Idara ya Ufundi, Bw. Paul Matumbi akiwasilisha taarifa za idara hiyo wakati wa kikao cha Baraza.

************************

Baraza la Wafanyakazi la Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) limesema limeridhishwa na utendaji kazi wa Taasisi hiyo na kuwapongeza watumishi kwa kuifanya Taasisi iendelee kutekeleza majukumu yake kwa ufasaha na ufanisi.

Hayo yamesemwa wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi PURA kilichofanyika hivi karibuni Jijini Arusha kwa lengo la kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji kutoka idara na vitengo vya Taasisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/22 na robo ya mwaka wa fedha 2022/23.

Akizungumza katika kikao hicho, Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam (Ms. Sara Rwezaula) ambaye ni mjumbe wa Baraza amesema kuwa utendaji wa Mamlaka hiyo umeendelea kuimarika mwaka hadi mwaka, jambo ambalo linastahili pongezi.

"Nipende kutumia fursa hii kuwapongeza wafanyakazi wote wa PURA kwa kufanya kazi kwa bidii kufikia malengo ya Taasisi. Kupitia Taarifa tulizozipokea na kujadili tumeona dhahiri kuwa Taasisi imekuwa na utendaji unaoridhisha. Pongezi nyingi pia kwa menejimenti ya PURA kwa kuendelea kuboresha mazingira ya kazi, jambo muhimu katika kufanikisha utendaji"

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi PURA ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo, Mha. Charles Sangweni amesema pongezi zilizotolewa ni chachu kwa wafanyakazi wa PURA kuendelea kufanya kazi kwa bidii zaidi ili kufikia malengo kama yalivyo katika Mpango Mkakati wa Taasisi.

"Nipende kutumia fursa hii kuwahimiza wafanyakazi wote wa PURA kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na kwa kuzingatia maadili ya utumishi wa umma. Tusibweteke kwa pongezi hizi bali ziwe kichocheo kwa sisi kufanya vizuri zaidi na zaidi" alieleza Mha. Sangweni.

Baraza la Wafanyakazi PURA linaundwa na wajumbe 34 na lilizinduliwa rasmi mwezi Novemba, 2020. Miongoni mwa wajumbe wa Baraza hilo ni Katibu TUGHE Taifa, Katibu TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, menejimenti ya PURA na wawakilishi kutoka idara na vitengo vya Taasisi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com