Mtaalamu wa maji kutoka Benki ya Dunia Rwegoshora Makaka akizungumza
Na Suzy Luhende, Shinyanga
Wananchi wa kata ya Ukenyenge wilayani Kishapu wameishukuru Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Wakala wa Maji Safi na Mazingira Vijijini (Ruwasa) kwa kuwapelekea mradi wa maji ya Ziwa Victoria, ambapo imesaidia kunusuru ndoa na kupunguza mimba za utotoni kutokana na kufuata maji umbali wa kilomita nne.
Hayo wameyasema leo Oktoba 7,2022 wananchi baada ya kutembelewa na wafadhili kutoka Benki ya Dunia, ambapo wamesema kabla ya kupata mradi wa maji wanawake walikuwa wakifuata maji umbali wa kilomita nne, hali ambayo ilikuwa ikisababisha ndoa nyingi kuvunjika na kuweza kushamiri kwa mimba za utotoni.
Monika Ngasa mkazi wa kijiji na kata ya Ukenyenge amesema wanaishukuru sana Benki ya Dunia kwa kushirikiana na wakala wa maji safi na mazingira Ruwasa, kwani walikuwa na changamoto kubwa, wanawake na watoto wakike walikuwa wakiamka usiku saa 10 hadi saa 11 ya usiku kufuata maji wakati mwingine watoto wa kike kubakwa na kusababisha mimba za utotoni.
"Lakini kwa sasa mradi huu wa maji ya Ziwa Victoria toka uanze katika kata yetu mimba za utotoni zimepungua,na ndoa zetu kwa sasa zimedumisha upendo, kwa sababu tulikuwa tukifuata maji tunapokawia tunapigwa na wakati mwingine tunapigana wanawake kwa wanawake huko mtoni kutokana na maji kutoka kidogo kidogo kwani kila mmoja alikuwa akitaka achote ili arudi nyumbani asipigwe na mme wake"amesema Monika ngasa.
Mwenyekiti wa bodi ya mradi huo kutoka kata ya Ukenyenge Kasimu Kishiwa amesema kabla ya kupata maji hayo hali ilikuwa ni mbaya watu walikuwa wanamaliza siku tatu bila kuoga lakini sasa hivi kila mtu anamelemeta kwa sababu maji yapo karibu ni kutoa Sh 50 tu kwa ndoo moja, na awali watu wengi walikuwa wakiugua tumbo, lakini sasa magojnwa ya tumbo yamepungua kutokana na kunywa maji safi na salama.
"Kuna changamoto ya baadhi ya maeneo wanaharibu miundo mbinu ya maji kwa kulima, kama kitongoji cha Mayanji waliharibu bomba lililopita kwenye shamba la miwa baada ya kufuatilia waligundua kuwa lilipasuka kwa bahati mbaya si makusudi, lakini wananchi wakiona uharibifu huo wanafidishia gharama ya maji yaliyomwagika hawakatai "amesema Kishiwa.
Kwa upande wake diwani wa kata hiyo Underson Mandia amesema anaishukiru sana Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Ruwasa kwa asilimia kubwa, kwani watu walikuwa wanatumia maji ya mchangani yasiyo salama, sasa wamepata maji ila kuna vitongoji vitatu havijafikiwa na maji lakini utaratibu wa kupeleka huko unaendelea ili kuhakikidha kata nzima inakuwa na maji ya kutosha.
Mandia amesema vijiji vinne vya kata ya Ukenyenge vimenufaika na maji ya Ziwa Victoria na kaya 156 wamefungiwa maji, lakini kuna vitongoji vinne havijafikiwa na maji, aidha kaya zilizovutiwa maji zinauziwa kwa unit moja Sh 1750, lakini wakati wanaanza walikuwa wakiuza unit moja sh 2500 baada ya kuona kipato ni kikubwa walipunguza ikawa sh 2000 baada ya kukaa tena wakashusha ikawa sh 1750 na wakikaa tena wanaweza wakashusha hadi 1500.
"Kwa kweli mmetusaidia sana, tunaomba muendelee kutushika mkono ili vitongoji vingine vifikiwe na maji ya ziwa victoria, mradi huu tunausimamia wenyewe, hivyo hatutaki kuumizana sisi kwa sisi ndio maana kila tunapokaa na kuona kipato tunaenda tunapunguza bei siku kwa siku ili kuhakikisha mwananchi haumii,mimi kama kiongozi wa wananchi nipo bega kwa bega na wananchi wangu ila naomba muwe mnawasomea wananchi taarifa ya mapato na matumizi",amesema Mandia.
Mhandisi wa maji Ruwasa wilaya ya Kishapu John Lugembe akisoma taarifa ya ujenzi wa mradi wa maji Ukenyenge amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza rasmi tarehe 15 Machi 2020 na ulikamilika na kuanza huduma kwa wananchi tarehe 25 Februari 2021 na chanzo cha maji hayo ni Ziwa Victoria kutoka bomba kuu KASHWASA.
Lugembe amesema ujenzi wa mradi huo umegharimu kiasi cha Sh 1. 1 Bilioni, kutoka programu ya malipo kwa matokeo, lengo la mradi huo ni kupunguza magonjwa ya milipuko kama vile kipindu pindu na homa ya matumbo inayosababishwa na kunywa maji yasiyo safi na salama na kuongeza upatikanaji wa maji ndani ya mita 400 kama ilivyo katika sera ya maji ya Taifa ya mwaka 2002.
"Tumetekeleza ujenzi wa matanki mawili ya kuhifadhi maji yenye ujazo wa lita 100, 000 na lita 50,000 katika minara ya mita 12 kwenye vijiji vya Negezi na Mayanji, vijiji vilivyofaidika ni Bulimba,Mayanji, Ukenyenge na Negezi ambao idadi yao ni wakazi 10,303 kati ya 11,074 ya wakazi wote sawa na asilimia 93 ambao wanapata huduma ya maji safi na salama", amesema Lugembe.
Kwa upande wake mtaalamu kutoka Benki ya Dunia Rwegoshora Makaka ameshauri kuwa katika mradi huo watambuliwe watu ambao hawajiwezi kabisa, hawana uwezo hawawezi kuzalisha na wa kulipia ndoo ya maji kama vile wazee wasaidiwe kuchota bure maji kwenye vituo vya maji ambavyo vipo karibu nao.
Naye Mshauri wa programu ya maji na usafi wa mazingira endelevu vijijini kutoka wizara ya Maji Kazimoto Edward amesema wanapokuwa na malalamiko waandike na kupeleka kujadiliwa na bodi, na bodi ikishajadili inaweza kupunguza bei ya maji ama kuongeza ili mradi maelewano yana kuwepo, pia inatakiwa kuendelea kuhamasisha ili kila mtu awe na maji nyumbani kwake idadi ya watu 156 bado ni ndogo sana.
Aidha mhandisi Mashaka Sitta ambaye ni mratibu kutoka wizara idara ya maji amewashauri watunze miundombinu ya maji ili iweze kudumu kwa muda mrefu na changamoto zinapotokea ziweze kutatuliwa kwa wakati.
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga
Dickson Kamazima akizungumza
Julieth Payovela Meneja Ruwasa mkoa wa Shinyanga akizungumza
Mtaalamu wa maji kutoka Benki ya Dunia Rwegoshora Makaka akizungumza
Wananchi wa kata ya Ukenyenge wilayani Kishapu wakimsikiliza mtaalamu kutoka Benki ya Dunia Rwegoshora Makaka akisisitiza jambo
Mtaalamu wa maji kutoka Benki ya Dunia Rwegoshora Makaka akizungumza na wananchi wa kata
Wadau wakiwa katika kata ya Ukenyenge wilaya ya Kishapu
Mshauri wa programu ya maji na usafi wa mazingira endelevu vijijini kutoka wizara ya Maji Kazimoto Edward akifuatilia taarifa ya mradi wa maji ya Ziwa Victoria
Diwani wa kata ya Ukenyenge Underson Mandia akizungumza baada ya kutembelewa na wataalamu kutoka Benki ya Dunia
Mhandisi wa maji Mashaka Sitta ambaye ni mratibu kutoka wizara ya maji akizungumza na wananchi wa kata ya Ukenyenge
Tenki la maji ya Ziwa Victoria
Neema Mwaifuge Afisa maendeleo ya jamii Ruwasa akizungumza baada ya kutembelewa na wataalamu wa Benki ya Dunia
Mtaalamu wa maji kutoka Benki ya Dunia Rwegoshora Makaka akizungumza
Wacheza ngoma wakiendelea kutoa burudani
Meneja wa Ruwasa wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Dickson Kamazima akizungumza
Ferister Kashinje mkazi wa kata ya Ukenyenge akishukuru kupatiwa maji safi na salama
Mwenyekiti wa bodi ya mradi wa maji ya Ziwa Victoria kutoka kata ya Ukenyenge Kasimu Kishiwa akishukuru kwa kupatiwa maji ya Ziwa Victoria
Viongozi mbalimbali wa mkoa wa Shinyanga, wizara ya Maji na Benki ya Dunia wakiwa katika kata ya Ukenyenge
Social Plugin