Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Bi. Zainab Abdallah
***
NA. ELISANTE KINDULU, BAGAMOYO
MKUU wa wilaya ya Bagamoyo Bi. Zainabu Abdallah amekipongeza chama Cha walimu Wilaya ya Bagamoyo kwa jitihada zake za kutafuta haki kwa njia ya maridhiano dhidi ya mwajiri.
Pongezi hizo zilitotolewa na mkuu huyo wa wilaya ambaye aliwakilishwa na Katibu Tawala wa wilaya ya Bagamoyo Bi. Kasilda Mgeni ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika kufungua mkutano mkuu wa chama hicho kwa wawakilishi wa mahala pa kazi wa wilaya ya Bagamoyo.
Akizungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho katika ukumbi wa shule ya sekondari Bagamoyo , Bi. Kasilda alisema chama Cha walimu Wilayani humo kimekuwa kikikaa meza moja mara kwa mara na mwajiri kwa lengo la kusaidia kuwaondolea kero walimu.
"Nampongeza Sana Katibu wenu. Amekuwa akija mara kwa mara ofisini kwangu kutafuta namna ya kuweza kutatua changamoto zinazowakabili . Na kwa kuwa Mimi ndiye msimamizi wa watumishi wote Wilayani huwa tunajadiliana vizuri na kufikia muafaka" alisema.
Hata hivyo Katibu Tawala huyo amewaasa walimu kuwa haki wanazozidai ziambatane na wajibu wanaoutumikia kwa mwajiri wao.
"Mimi Ni mjumbe wa kamati za maamuzi zinazojadili mienendo mibaya ya walimu. Huwa nachukizwa na tabia za uzinzi, ulevi kupindukia pamoja na utoro kazini", alisema.
Katika taarifa yao kwa Mgeni rasmi, Mwenyekiti wa Chama hicho ,Hamisi Kimeza na Katibu wake Mwlimu Shaaban Tessua walimueleza Katibu Tawala huyo kuwa walimu Wilayani Bagamoyo wanakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Zikiwemo kuchelewa kulipwa mapunjo ya mshahara (arreas), uhaba wa nyumba za kuishi walimu pamoja na changamoto ya malipo ya fedha za uhamisho.
Mkutano huo ulihudhuriwa na maafisa elimu msingi na Sekondari kutoka halmashauri ya Bagamoyo na Chalinze, kaimu Katibu wa tume ya utumishi wa walimu Wilaya ya Bagamoyo, afisa utumishi wa wilaya ya Bagamoyo na viongozi wa CWT kutoka mkoa wa Pwani.
Social Plugin