Wakazi wa kijiji cha Shipalo, eneo la Malava, kaunti ya Kakamega nchini Kenya wamepigwa na bumbuwazi baada ya jamaa kudaiwa kumuua mke wake kufuatia ugomvi wa nyumbani.
Jonathan Shikulu anaripotiwa kugombana na mke wake Faith Nanzala, baada ya kumzuia kuoa mke wa pili.
Katika tukio hilo la Jumapili, Oktoba 9, ugomvi wao ulichacha huku Shikulu akiripotiwa kuanza kumpiga Nanzala mwenye umri wa miaka 31, hadi kumuua.
Majirani waliambia runinga ya Citizen kuwa wakati vita hivyo vilipokuwa vikiendelea, mama mkwe wa Nanzala alikuwa akimrushia cheche ya matusi huku akimshabikia mwanawe kuendelea kumpiga.
Katika njia ya kuficha uovu wake, jamaa huyo alipogundua mwanamke huyo amekwenda jongomeo, aliambia familia yake kwamba alijitoa uhai.
Mwili wa marehemu ulipelekwa katika Hifadhi ya Maiti ya Webuye huku uchunguzi kuhusu tukio hilo ukiendelea.
Kwa upande mwingine, Shikulu ambaye anachukuliwa kuwa mshukiwa mkuu, alikamatwa na kufungiwa katika Kituo cha Polisi cha Malava kuhojiwa.
Social Plugin