Timu ya Kamba wanaume ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kiwavuta Timu ya Kamba ya Bunge (hawapo pichani) wakati wa Michuano Shirikisho la Michezo ya Wiraza na Idara za Serikali na Mikoa (SHIMIWI) inayoendelea jijini Tanga. Timu ya Uchaguzi ilishinda mchezo huo kwa mivuto yote miwili. (Picha na Mroki Mroki).
Michuano Shirikisho la Michezo ya Wiraza na Idara za Serikali na Mikoa (SHIMIWI) imezidi kurindima katika viunga vya jiji la Tanga ambapo Timu za Kamba za Tume ya Taifa ya Uchaguzi zimeendeleza ubabe wao kwa timu za kundi E wanaume na kundi F Wanawake.
Katika michezo ya leo Oktoba 4,2022 timu ya Kamba ya Uchaguzi wanaume wamewahenyesha na kuchukua lama tatu kutoka kwa Mhimili wa Bunge.
Mchezo huo ambao awali ulikuwa unaonekana kuwa mgumu kwa pande zote mbili kutokana na aina ya wachezaji waliopo lakini ulikuwa mwepesi kwa miamba ya Uchaguzi.
Katika mchezo mwingine Timu ya wanawake wa Uchaguzi ilipata alama tatu za mezani kufuatia wapinzani wao RAS Ruvuma kuingia mitini katika mchezo wa kundi F.
Baada ya matokeo hayo sasa Timu ya Wanawake wa Uchaguzi imebakiza mchezo dhidi ya Wizara ya Madini ambapo wanaume wanasubiri kukutana na RAS Shinyanga.
Kundi la Kamba wanaume lina timu za Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano Afrika Mashariki, Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, RAS Shinganga na RAS Manyara.
Upande wa Kundi F timu ya Kamba wanawake kuna timu za Tume ya Taifa ya Uchaguzi, RAS Dodoma, RAS Ruvuma na Wizara ya Madini.