Helena Hungoli na mtoto wake Safari Bidale, waliofanyiwa upasuaji
**
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, imefanya upasuaji rekebishi kwa mama Helena Hungoli na mtoto wake Safari Bidale wakazi wa mkoa wa Manyara ambao walimuomba msaada wa matibabu Rais Samia, mama Helena na mwanaye walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya ugonjwa usiokuwa na tiba maalum duniani.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 19, 2022, Mkurugenzi wa hospitali hiyo Profesa Mohamed Janabi, amesema mama huyo na mtoto wake walikuwa wanakabiliwa na changamoto ya ugonjwa ambao hauna tiba maalum duniani na kitaalam unaonesha kwamba ugonjwa huo umeanzia kwenye vinasaba vya mama mzazi na ndipo ukaenda mpaka kwa mtoto wake.
Naye daktari bingwa wa upasuaji rekebishi Dkt Ibrahim Nkoma, amesema mama huyo na mtoto wake walikuwa na uvimbe ambao ulikuwa ukisababisha matatizo kwenye maisha yao ya kila siku ambapo mama peke yake amelazimika kufanyiwa upasuaji mkubwa kwa mara mbili kutokana na ukubwa wa uvimbe aliokuwa nao kwenye uso huku mtoto wake akifanyiwa upasuaji mara moja.
Akizungumza mara baada ya upasuaji huo Safari Bidale, ambaye ni mtoto wa mama Helena Hungoli amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan huku akiwasihi Watanzania wengine wenye tatizo kama hilo kujitokeza na kupatiwa msaada wa matibabu badala ya kukata tamaa na kukaa nyumbani.
CHANZO - EATV
Social Plugin