Mwanaume mmoja Mkazi wa Dar-es-Salaam aliyefahamika kwa jina la James Merikiori amejinyonga hadi kufa akiwa nyumbani kwa kaka yake eneo la Ikindwa, Kata ya Mapambano Manispaa ya Tabora huku Jeshi la Polisi likitoa tahadhari kwa wananchi kutafuta namna nzuri ya kushughulikia changamoto zao za maisha zinapowakabili badala ya kujichukulia uamuzi wa kujitoa uhai.
Mwili wa marahemu James ulikutwa chumbani ukiwa unaning’inia kwenye paa la nyumba baada ya kudaiwa kujinyonga kwa kutumia shuka na mara baada ya polisi kuwasili eneo la tukio walibaini kuwepo kwa ujumbe kwenye simu ya marehemu aliokuwa akiuandika kabla ya kutekeleza tukio hilo la kujiua.
Kaka wa marehemu Boniface Merikiori amesema mdogo wake ambaye aliiacha familia yake mke na watoto jijini Dar-es-Salaam alifika Tabora kwaajili ya kutafuta kazi na kazi aliyoikusudia ilikuwa ni kuendesha bodaboda akidai kwamba maisha Dar Es Salaam yamekuwa magumu.
Mkaguzi wa Polisi Wilaya ya Tabora mjini, Josephat Sanya akiwa kwenye tukio hilo alipata wasaa wa kuzungumza na wananchi ambao walifika kushuhudia tukio hilo ambapo aliwatahadharisha kujenga tabia ya kuwashirikisha watu wao wa karibu wakati wanapokabiliana na changamoto za kimaisha badala ya kuchukua uamuzi wa kujiua kwakuwa siyo suluhisho la matatizo yanayowakabili katika maisha.
Social Plugin