Mshindi wa kiti cha uenyekiti wilaya ya Kahama kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) Thomas Muyonga akiwashukuru wajumbe baada ya kumchagua kwa kura nyingi.
Na Kareny Masasy, Kahama
THOMAS Muyonga ameshinda nafasi ya mwenyekiti wilaya ya Kahama kupitia chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kupata kura 1,722 dhidi ya wapinzani wake Costantine Makoye aliyepata kura 179 na Michael Kulwa aliyepata kura 127.
Uchaguzi huo ulianza jana tarehe 1 mwezi Oktoba na kukamilika leo tarehe 2 mwezi Oktoba mwaka 2022 kwa kuendelea kuchagua kamati ya utekelezaji wilaya huku wajumbe takribani 2028 walijitokeza kupiga kura kwa nafasi ya mwenyekiti wilaya.
Msimamizi wa uchaguzi huo James Kusekwa ametangaza matokea na majina ya waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali ambapo alimtangaza mwenyekiti Thomas Muyonga kuwa mwenyekiti wa CCM wilaya baada ya kutetea kiti hicho kwa awamu ya pili sasa.
Kusekwa amemtangaza katibu itikadi na uenezi Joackim Simbila aliyetetea kiti hicho kwa kupata kura 151 dhidi ya mpinzani wake Mola Zabron aliyepata kura 72 huku wajumbe waliopiga kura kwenye nafasi hiyo wakiwa 267.
Aidha Kusekwa aliendelea kutangaza makundi ya uwakilishi ambapo kundi la vijana mshindi alikuwa Godfrey Simba aliyepata kura 261 kati ya kura 263, kundi la wazazi Julias Lugobi aliyepata kura 203 huku kundi la uwakilishi umoja wa wanawake wa chama cha Mapinduzi (UWT) alichaguliwa Juliana Kajala.
Baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo mshindi Thomas Muyonga alipata nafasi ya kuwasalimia wajumbe na kueleza kuwa uchaguzi umekwisha wanatakiwa wasonge mbele kazi iendelee na kuvunja makundi yaliyokuwepo.
Muyonga amewashukuru wajumbe kwa kuwa wavumilivu kwa zoezi la uchaguzi lililoanza jana na kumchagua kuendelea kuongoza kiti hicho kwa kipindi cha miaka mitano tena.