Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MUYONGA ATOBOA TENA UENYEKITI CCM KAHAMA MJINI

 

Mshindi wa kiti cha uenyekiti wilaya ya Kahama kwa Chama cha Mapinduzi (CCM) Thomas Muyonga  akiwashukuru wajumbe  baada ya kumchagua kwa kura nyingi.

Na Kareny  Masasy, Kahama

THOMAS Muyonga  ameshinda nafasi ya  mwenyekiti  wilaya ya Kahama kupitia chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kupata kura 1,722 dhidi ya  wapinzani wake Costantine  Makoye aliyepata kura  179 na  Michael Kulwa aliyepata kura 127.

Uchaguzi huo ulianza jana tarehe 1 mwezi Oktoba na kukamilika leo tarehe 2  mwezi Oktoba mwaka 2022   kwa kuendelea   kuchagua  kamati ya utekelezaji  wilaya huku wajumbe takribani  2028 walijitokeza kupiga kura kwa nafasi ya mwenyekiti wilaya.

Msimamizi wa uchaguzi huo  James Kusekwa ametangaza  matokea na majina ya waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali ambapo  alimtangaza mwenyekiti Thomas Muyonga kuwa mwenyekiti wa CCM wilaya baada ya  kutetea kiti hicho kwa awamu ya pili  sasa.

Kusekwa  amemtangaza  katibu  itikadi na uenezi   Joackim  Simbila  aliyetetea kiti hicho  kwa kupata kura  151 dhidi ya mpinzani wake Mola Zabron aliyepata kura  72  huku wajumbe waliopiga kura kwenye nafasi hiyo  wakiwa 267.

Aidha Kusekwa aliendelea kutangaza makundi ya uwakilishi ambapo kundi la vijana mshindi alikuwa Godfrey Simba  aliyepata kura 261 kati ya kura 263, kundi la wazazi  Julias Lugobi aliyepata kura  203 huku kundi la uwakilishi  umoja wa wanawake wa chama cha Mapinduzi  (UWT)  alichaguliwa Juliana  Kajala.

Baada ya kutangazwa kwa matokeo hayo  mshindi  Thomas Muyonga alipata nafasi  ya kuwasalimia wajumbe na kueleza kuwa uchaguzi umekwisha wanatakiwa wasonge mbele kazi iendelee na kuvunja makundi yaliyokuwepo.

Muyonga amewashukuru wajumbe kwa kuwa wavumilivu kwa zoezi la uchaguzi lililoanza jana  na kumchagua kuendelea kuongoza kiti hicho kwa kipindi cha miaka mitano tena.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com