Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WATU WATATU WAUAWA KOLANDOTO SHINYANGA, ALIYEANZA KUUA ACHOMWA MOTO

 


Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi akizungumza na waandishi wa habari kuhusu tukio la mauaji Kolandoto Shinyanga.

Na Halima Khoya, SHINYANGA

Watu wawili ambao ni Nicholaus Leonard na Badmalta Melikiad, wameuawa kwa kupigwa na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili wao na wengine watatu kujeruhiwa, na mtu ambaye hajafahamika akidaiwa kurukwa na akili ambaye naye ameuawa kwa kupigwa kisha kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali.



Tukio hilo limetokea jana Oktoba 2 ,2022 katika Kata ya Kolandoto Manispaa ya Shinyanga majira ya saa moja jioni.

Akisimulia tukio hilo leo mmoja wa majeruhi Daniel Emmanuel, amesema mtu huyo alivamia katika nyumba ya bwana Nicholaus Leonard, na kuwakuta mke wa Nicholaus ambaye ni Lucia Luhende akisukana na Rafiki yake Badmalta ndipo akaanza kuwashambulia.

Anasema wakati akiwashambulia akajitokeza kuwasaidia ndipo na yeye akapigwa kichwani na kitu kizito kichwani akapasuka na kuanza kuomba msaada, huku mmoja wa wanawake hao Badmalta akipigwa vibaya na kusabisha kifo chake papo hapo.

“Nilienda kuwasaidia baada ya kusikia kelele katika nyumba hiyo ya bwana Nicholaus, ambapo mtu huyo alikuwa amefunga mlango na mimi nilivyofika nikafungua mlango lakini bahati mbaya jamaa alikuwa amejibanza katika kona nilivyoingia tu akanipiga kichwani nikaanguka chini,”Amesema Daniel.

“Wakati vurugu hizo zikiendelea na mimi kuelemewa kushindwa kutoa msaada kutokana na kuvuja damu nyingi, mume wa Lucia Luhende bwana Nicholaus Leonard aliingia ndani kutoa msaada, lakini na yeye akapigwa kichwani akaanguka chini na kupoteza maisha papo hapo,”anaongeza.

Kwa upande wake Mke wa Marehemu Lucia Luhende, amesema yeye alifanikiwa kutoka nje wakati mtu huyo akiendelea kumshambulia Rafiki yake, ndipo mume wake akaingia ndani ili kumuokoa lakini hakufanikiwa kutokana na kupigwa vibaya kichwani kisha akapoteza maisha.

Naye Diwani wa Kolandoto Mussa Andrew, amesema baada ya kupokea taarifa alifika eneo la tukio na kumkuta jamaa akiwa bado ndani ya nyumba hiyo, akapiga simu kuomba msaada Polisi, lakini wananchi wenye hasira kali walifanikiwa kumtoa nje na kisha kuanza kumkimbiza.

Anasema wananchi hao walifanikiwa kumkamata na kisha kuanza kumpiga kwa mawe na baadae kumchoma moto.

Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kolandoto Dk. Joseph Wallace, amethibitisha kupokea miili ya marehemu watatu akiwamo na kijana huyo ambaye aliuawa na wananchi, pamoja na majeruhi watatu huku mmoja akipewa rufaa ya kwenda Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo la mauaji, na kutoa wito kwa wananchi wakimuona mtu analeta taharuki watoe taarifa ili kuzuia maafa yasitokee.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com