Mzee wa makamo kutoka wadi ya Mwingi magharibi, Kitui nchini Kenya kwa sasa anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Migwani baada ya kumuua mwanawe.
Inasemekana mshukiwa aliyejulikana kwa jina la Mwendwa, alitumia shoka kumuua mtoto wa miaka 14, Mumo Mwendwa ambaye mpaka kifo chake alikuwa ni mwanafunzi wa shule ya msingi ya Kyomo katika darasa la nane.
Esther Mwendwa, mkewe anayefanya kazi Kibwezi, alisema hakuwa nyumbani wakati kisa hicho kilipotokea na alifahamishwa na jamaa kuhusu kufariki kwa mwanawe.
“Baba yake alikuwa amemtuma kuchota maji mtoni, badala yake Mumo alienda kucheza na marafiki,” alisema.
Mtoto huyo alikimbia alipomwona babaake ambaye kulingana na mkewe alisema alikuwa ni mtu mwenye vurugu kufuatia tabia yake ya kutumia dawa za kulevya.
“Alimkatakata hadi kumuua kwa kutumia shoka na visu,” alisema.
Esther pia aliongeza kuwa mwezi uliopita, alimpiga kichwani na kumjeruhi vibaya.
Alisema mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Migwani.
“Mwanangu alikufa kifo cha maumivu sana na ninaiomba serikali kuingilia kati na kuhakikisha haki inatendeka,” aliongeza
Florence Muli, binamu wa marehemu alisema kuwa kisa hicho kilitokea mwendo wa saa tano za usiku wa Jumapili.
Alisema alikuwa amefunga nyumba kutoka ndani na alipiga kelele kuomba msaada kutoka kwa majirani.
Benard Mwangangi kaka yake mkubwa alisema usiku huo huo, alisikia kelele nyingi kutoka kwa kaka yake na kudhani ni tabia yake dhahiri ya kumpiga mwanawe.
Alisema amekuwa na uadui sana na watu wengi hata waliogopa kutembelea nyumba yake.
“Baada ya kumsikia akipiga kelele, mara moja nilimsikia mwanawe, Mumo akipiga kelele kuomba msaada,” alisema
Muda mfupi baadaye, alisikia baba yao akigombana naye na akamwambia baba yake anataka kumuua mwanawe.
Mwangangi alipoenda kwenye nyumba hiyo, alimkuta mtoto wa miaka 14 akiwa amelala amefariki huku mshukiwa akiwa amefungwa kamba na wananchi waliokuwa wakisubiri maafisa wa polisi.
Pia aliongeza kuwa mkewe amekuwa akiishi kwa hofu kufuatia visa kadhaa vya unyanyasaji wa nyumbani.
Akithibitisha kisa hicho, chifu wa eneo hilo Grace Mwikali Muli alisema mwanaume huyo kwa sasa anazuiliwa katika kituo cha Polisi cha Migwani akisubiri uchunguzi zaidi.
Social Plugin