Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI MASANJA AWATAKA WAKUU WA WILAYA KUSIMAMIA IPASAVYO MAENEO YA HIFADHI


************ 

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) amewataka Wakuu wa Wilaya nchini kusimamia vyema maeneo ya hifadhi ili kuepusha migogoro baina ya shughuli za kibinadamu na hifadhi. 

Ameyasema hayo Oktoba 11, 2022 mkoani Rukwa wakati wa Ziara ya Mawaziri wa Kisekta ya kutatua migogoro ya Ardhi katika vijiji 975 nchini. 

“Kila mtu akisimamia eneo lake vizuri hii migogoro itapungua sana ama kuisha lakini tukisubiri Serikali iseme au Kamati ya Mawaziri iseme, maeneo ya hifadhi yatakwisha” Mhe. Masanja amesisitiza. 

Amefafanua kuwa changamoto kubwa inayoipata Serikali kwenye uhifadhi ni muingiliano wa shughuli za kibinadamu na utunzaji wa maeneo ya hifadhi ambapo wananchi wanaanzisha vijiji katikati ya hifadhi. 

Mhe. Masanja amewaelekeza Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi na Watendaji wa Vijiji kuhakiki wahamiaji wanaoingia katika maeneo yao ili kujua sababu inayowafanya waanzishe vijiji katika hifadhi na pia watoe maelekezo ya kutosha kwa wananchi kuhusu umuhimu wa uhifadhi na kuwasimamia ili kuondokana na migogoro ya ardhi. 

“Ifike mahala wananchi wafahamu umuhimu wa uhifadhi na shughuli za kibinadamu” ameongeza. 

Amesema endapo hifadhi zitaendelea kuvamiwa changamoto za mabadiliko ya tabia ya nchi zitaendelea kujitokeza. 

Aidha, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa jinsi ambavyo ameelekeza migogoro hiyo itatuliwe ambapo kwa sasa hifadhi zinaheshimika na wananchi wanaendelea na maisha yao ya kila siku. 

Ziara ya Kamati ya Mawaziri wa Kisekta itaendelea katika mkoa wa Katavi tarehe 12 Oktoba kabla ya kuelekea Kigoma Oktoba 13,2022.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com