Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara NHC, William Genya
Meneja habari na Uhusiano wa NHC, Muungano Saguya
Na Dotto Kwilasa, DODOMA
SHIRIKA la Nyumba la Taifa (NHC), linatarajia kuzindua sera ya ubia ya ushirikiano na sekta binafsi itakayowezesha utakelezaji wa miradi na uboreshaji wa majengo yenye hali mbaya yanayomilikiwa na shirika hilo.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara NHC, William Genya amesema hayo Leo Jijini hapa wakati akizungumza na Waandishi wa habari na kueleza kuwa ubia huo utawezesha uboreshaji majengo yenye hali mbaya ya NHC ya mitaa mbalimbali ikiwemo ya Kariakoo na Upanga.
Amesema hatua ya uzinduzi wa sera hiyo, itafanyika Novemba 14 mwaka huu huku ikitarajiwa kutoa fursa kwa NHC kuingia ubia na sekta ya binafsi kwa ajili kujenga miradi ya maendeleo katika viwanja inavyovimiliki na kuwa kisasa hali itakayo toa fursa ya familia nyingi kupata makazi na maeneo ya biashara.
“Sera imeboreshwa kwa kuongeza vitu vikubwa vinne ikiwemo kutumia ardhi kama mtaji, sera nyingine ni NHC inaweka ardhi na mbia anaweka fedha halafu wanatekeleza mradi kwa pamoja na hii ni kwa miradi mikubwa ya kuanzia sh.bilioni 50,"amesema.
Mkurugenzi huyo pia ametaja sera nyingine kuwa ni kujenga jengo kati ya shirika na wabia kisha kuuzwa na mapato kugawanywa na sera ya mwisho ni shirika kutoa ardhi kwa mkataba wa miaka 10 na mbia anajenga, baada mkataba kuisha jengo linakuwa mali ya shirika.
“Sera hii ina lenga kuwapa fursa wawekezaji binafsi wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza nchini, ambapo itafungua milango ya uwekezaji kwenye sekta ya nyumba ili kuunga mkono maono maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuvutia uwekezaji nchini kwa kuruhusu sekta binfasi ambayo ni injini ya kuleta maendeleo ili iwekeze mitaji yao katika kujenga uchumi wa Taifa letu,” amesema
ameongeza kuwa uzinduzi huo una lengo la kuwaalika Watanzania kushiriki kwenye Sera hiyo iliyoanzishwa na shirika tangu mwaka 1993 na kufanyiwa maboresho kadhaa kulingana na wakati husika.
Katika hatua nyingine Genya amesema tangu kuanza kwa utaratibu huu jumla ya miradi 111 ilitekelezwa ikiwa na thamani ya sh.bilioni 300 ambapo katika miradi hiyo, miradi 81 yenye thamani ya sh.bilioni 240 imekamilika na kuanza kutumika na miradi 30 yenye thamani ya sh.bilioni 60 inaendelea kukamilishwa.
amefafanua kuwa miradi hiyo imechangia upatikanaji wa ajira, kuboresha mandhari ya miji, kuongeza mapato ya shirika, kuongeza wigo wa kodi za serikali, kuongeza maeneo kwa ajili ya biashara na makazi.
“Katika uzinduzi huo mkubwa tunakusudia kuwa na washiriki takribani 600 kutoka tasisi mbalimbali za serikali na binafsi, vyama na bodi za kitaalum pamoja na wawekezaji binafsi wa ndani na nje ya nchi ambao wamealikwa,”amesema
Kwa upande wake Meneja habari na Uhusiano wa NHC, Muungano Saguya amesema uzinduzi wa sera hiyo utafanyika Novemba 14 mwaka huu katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Social Plugin