Mkurugenzi wa Uwekezaji katika Ofisi ya Msajili wa Hazina, Bi.Lightness Mauki akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 26,2022 Jijini Dodoma
*************
*Thamani ya uwekezaji kwenye Mashirika ya Umma wafikia trilioni 70/-
Na Mwandishi Maalumu, Dodoma
OFISI ya Msajili wa Hazina (OMH) imesema kumekuwa na mafanikio makubwa katika usimamizi na uendelezaji wa uwekezaji uliofanywa na Serikali katika mashirika ya umma 287, ambao thamani yake ya uwekezaji imepaa na kufikia Shilingi trilioni 70.
Kati ya mashirika hayo, taasisi 237 umiliki wake ni zaidi ya asilimia 51 kwa mujibu wa Sheria ya Mashirika ya Umma Sura 257, taasisi 40 zinamilikiwa na Serikali kwa hisa chache na taasisi 10 za nje ya nchi.
Hayo yamo katika Taarifa ya Ofisi ya Msajili wa Hazina kuhusu utekelezaji wa majukumu mbalimbali na mwelekeo wa utekelezaji katika kipindi cha mwaka 2022/2023 iliyowasilishwa jana na Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Umma katika Ofisi hiyo, Lightness Mauki kwenye ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo mjini Dodoma.
Imeeleza kuwa, mapato yamekuwa yakiimarika mwaka hadi mwaka na kufikia Juni 30, 2022, ofisi hiyo ilikuwa imekusanya kiasi cha Shilingi bilioni 852.98 sawa na asilimia 109.5 ya lengo. Awali lengo lilikuwa kukusanya Shilingi bilioni 779.03. Ongezeko la mapato hayo ni asilimia 33.5 zaidi ya kiasi kilichokusanywa Juni 30, 2021 ambacho kilikuwa ni Shilingi bilioni 638.87.
Mauki alisema katika kutekeleza majukumu yake ya kisheria pamoja na mambo mengine ana jukumu la kukusanya mapato yasiyo ya kodi ambayo yanajumuisha gawio, michango ya 15% ya mapato ghafi na mapato mengineyo.
"Huu ni ufanisi mkubwa, unaotia moyo na ambao haujawahi kufikiwa. Ufanisi huu umechangiwa na kuimarisha usimamizi, ufuatiliaji na tathmini ya uwekezaji wa mitaji ya Umma, hatua za makusudi zilizochukuliwa na serikali katika kukuza mapato na kudhibiti matumizi pamoja na kuongezeka kwa shughuli za ufuatiliaji katika taasisi, mashirika ya umma na Kampuni ambazo Serikali inamiliki hisa chache," alisema Mauki.
Ofisi imeishukuru Serikali ya awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi thabiti wa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya msingi ya Msajili wa Hazina kufanyika kwa ufanisi na endelevu.
Alisema chini ya usimamizi wake, upanuzi wa Kiwanda cha Sukari cha Kilombero unaolenga kupunguza kwa kiasi kikubwa uhaba wa sukari nchini, unaendelea vyema. Serikali na wanahisa wenza (Illovo Group) wapo katika kutekeleza mradi mkubwa wa upanuzi wa kiwanda hicho kwa gharama ya Sh bilioni 571.6. Uwekezaji huo unatarajiwa kuzalisha sukari tani 144,000 na kufikia tani 271,000 kiwandani hapo kutoka tani 127,000 za sasa.
“Ndugu wana habari utekelezaji wa mradi huu tayari umeanza na unatarajiwa kuwa na mafanikio makubwa kwa njia ya kuongeza ajira, kuinua kipato kwa wananchi wanaozunguka eneo hilo, gawio kwa wanahisa na kichocheo cha uchumi kwa ujumla,” alisema Msajili.
Mafanikio mengine ni kununua na kufufua shamba la KPL Mngeta kutoka kwa Meneja Mfilisi kwa Dola za Marekani milioni 7.40. Shamba hili lenye thamani ya Shilingi bilioni 152.19 ni uwekezaji mkubwa wa Serikali uliokabidhiwa Kampuni ya SUMA JKT ambayo inajishughulisha na vitega uchumi mbalimbali ikiwemo kilimo cha biashara.
Aligusia pia mafanikio ya kuimarika utendaji wa kampuni ambazo Serikali ina umiiki wa hisa chache, akitolea mfano utendaji wa Benki ya NBC ambayo imeongeza faida kabla ya kodi kutoka Shilingi bilioni 7 mwaka 2020 hadi Shilingi bilioni 60 mwaka 2021, sawa na ongezeko la asilimia 757. Ukuaji huu wa faida umewezesha benki hii kutoa gawio kwa serikali Shilingi Billioni 4.5 kiasi ambacho hakijawahi kufikiwa.
Aidha, mapato kutoka Kampuni ya Airtel yameongezeka kutoka kiasi cha Shilingi bilioni 34.66 mwaka 2020/21 hadi kiasi cha Shilingi bilioni 104.22 mwaka 2021/22. Mapato haya yanajumuisha ulipaji wa gawio na utekelezaji wa makubaliano maalumu ya wanahisa.
Aidha, Benki ya NMB imetoa kwa Serikali gawio la kiasi cha Shilingi Bilioni 30.7 kutoka Shilingi Bilioni 21.7 ya mwaka 2020/21. Msajili alisema mafanikio hayo makubwa yametokana na uimarishwaji wa mahusiano ya kiutendaji baina ya wanahisa.
"Serikali kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali imefanikiwa kufanya majadiliano nje ya Mahakama na kumaliza Shauri lililofunguliwa na Benki ya Exim Tanzania dhidi ya TFC katika Mahakama ya Biashara baada ya Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) kushindwa kulipa deni la mkopo lililokuwa limefika Dola za Marekani milioni 6.7.
“Kupitia majadiliano hayo, Serikali imelipa kiasi cha Dola za Marekani milioni 2.7 na hivyo kuokoa kiasi cha Dola za Marekani milioni 4.0 pamoja na mali za TFC zilizowekwa kama dhamana ambazo ni maghala yaliyopo Mwanza, Iringa, Tabora na Jengo la Ofisi lililopo barabara ya Chole, Oysterbay jijini Dar es Salaam," alisema Mauki.
Aliongeza kuwa, Ofisi ya Msajili wa Hazina itaendelea kudhibiti matumizi ya Mashirika ya Umma kwa kuanzisha Mfumo wa Mipango na Bajeti (PLANREP) kwa Taasisi, Wakala za Serikali na Mashirika ya Umma na kwamba Taasisi zote zimefanikiwa kuingiza Taarifa zao za bajeti kwa ajili ya uchambuzi, idhini na kuanza kufanya matumizi kuanzia mwezi Julai 2021.
Kuhusu umiliki hisa katika Kampuni za Madini zisizopungua asilimia 16, alisema Msajili wa Hazina ameendelea kutekeleza Kifungu cha 10 cha Sheria ya Madini, Sura 123 kuhusu hisa zisizohamishika umeendelea kuiwezesha Serikali kuwa na hisa katika baadhi ya kampuni za madini na pia kuongeza umiliki kwenye baadhi ya kampuni.
Ofisi ya Msajili wa Hazina kama msimamizi mkuu wa uwekezaji wa Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utendaji wa Taasisi na Mashirika ya Umma ili kuhakikisha Serikali inapata marejesho (return) ya uwekezaji wake, sambamba na kuongezeka kwa mapato yasiyo ya kodi ili kusaidia miradi ya maendeleo kwa faida ya Taifa na wananchi wote kwa ujumla.