ROMBO KUTUMIA SOKO LA KIMATAIFA KUUZA NDIZI ILI KUONGEZA KIPATO CHA WAKULIMA.

 
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda

Na Mathias Canal, KILIMANJARO

KATIKA  kuimarisha sekta ya Kilimo  imeelezwa kuwa kuna umuhimu wa kutumia soko la kimataifa kuuza ndizi ili kuongeza kipato cha wakulima.

Mbunge wa Jimbo la Rombo ambaye pia ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof Adolf Mkenda amesema hayo jana 3,Octoba 2022 katika kata ya Masera Wilayani Rombo Kilimanjaro wakati akizindua mafunzo ya siku saba ya uzalishaji wa zao la ndizi na maadhimisho ya wiki ya huduma kwa wateja yanayoongozwa na kauli mbiu isemayo "Ndizi kwa Afya bora na Kipato Zaidi".

Prof Mkenda amesema kuwa hapa Tanzania ndizi ni zao la kupika na matunda hivyo kama likizalishwa na kutumika vizuri litabadili uchumi wa nchi.

Waziri Mkenda amewema kuwa kitafanyika kikao maalumu "Roundtable" kwa wadau wa ndizi Wilayani Rombo ili kujadili mikakati ya kukuza kilimo cha kisasa cha ndizi.

Ameongeza kuwaa kupitia zao hilo bado hakujapatikana mapato ya kutosha kutokana na kutokuwepo soko la uhakika.

“Ni lazima tuangalie ndizi kama zao la biashara ambalo litatupa chakula cha uhakika, Tulifanya mkutano wa zao la ndizi Moshi na tulipanga kufanya mkutano wa kitaifa wa mkakati wa kukuza zao hilo nchi nzima, lakini ndizi bado ni uti wa mgongo wa uchumi wa wilaya ya Rombo,” Amekaririwa Prof Mkenda

Amesema zao la ndizi ni muhimu kwa sababu linatoa uhakika wa chakula licha ya kuwa kahawa ni muhimu lakini kama haina soko huwezi kuila kama ilivyo ndizi.

“Usipopata soko la ndizi maana yake huwezi kuwa na chakula nyumbani, hivyo kuwataka watu kutambua kuwa zao hilo ni kubwa la kibiashara.

Ametoa mfano kuwa nchi ya Amerika Kusini ya Ecuador inauza ndizi kwa wingi na Taifa hilo linapata zaidi ya Dola za Marekani Bilioni mbili kwa mwaka ambapo inakuwa zaidi ya fedha ambazo Tanzania inapata kwa kuuza kahawa nje ya nchi.

Amesisitiza kuwa kama ndizi zitalimwa kwa wingi na tija kutakuwa na uhakika wa chakula nchini, na zitasaidia maeneo yenye ukame na zitauzwa ndani na nje ya nchi.

Katika hatua nyingine ameipongeza Taasisi inayojishughulisha na Kilimo cha maua, matunda na mbogamboga (TAHA) kwa kudhamini mafunzo hayo ambayo yatafanyika kwa siku saba kwa lengo la kuwaongezea uelewa na uwezo wakulima kuzalisha kwa wingi na tija zao la ndizi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post