Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SAMAF NA ITEL ZAUNGANA KURUDISHA TABASAMU KWA KITUO CHA WATOTO WENYE ULEMAVU CHA AMANI NA MIHAYO




Na Mwandishi wetu,Morogoro 

UMOJA wa waandishi wa habari wanawake Dar es Salaam chini ya asasi ya sauti ya matumaini Foundation SAMAF kwa kushirikiana na Kampuni ya Simu ya Itel  wametembelea Kituo cha kulelea watoto yatima wenye ulemavu na wanaoishi katika mazingira magumu cha Amani na Mihayo vilivyopo  kata ya Chamwino Mkoani  Morogoro na kutoa misaada mbalimbali ikiwemo taulo za kike pamoja na chakula kwa lengo la kurudisha  tabasamu kwa watoto hao.


Akizungumza wakati wa kutoa msaada huo,Mwanzilishi wa Umoja wa umoja huo,Penina Malundo alisema taasisi yao inaendelea kuhakikisha inarudisha tabasamu kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na wale wenye ulemavu kwa kuwasaidia vitu mbalimbali ikiwemo kuwapa elimu ya Afya,Kujitambua pamoja na masuala ya ukatili wa kijinsia ili kuweza kuwasaidia katika makuzi yao.


Alisema mbali na elimu hiyo pia wamekuwa wakitoa taulo za kike kwa mabinti hao za kipindi cha miezi sita  ili ziweze kuwasaidia mabinti hao kuweza kupata hedhi salama ambayo itawafanya kutokuwa wanyonge kwa kuendelea na shughuli zao kama masomo.


"Hii sasa ni awamu ya tatu kwa mwezi huu wa tisa kutoa elimu ya afya ya uzazi,kujitambua na ukatili wa kijinsia tumeweza kufikia shule tatu ikiwemo shule ya msingi Buguruni Viziwi,Maweni,Kigamboni,Vijibweni na Kituo cha Amani na Mihayo mkoani Morogoro jumla ya mabinti 200 tumeweza kuwafikia na kampeni yetu ya ithamini na ilinde kesho yangu,"alisema na kuongeza


"Mkoani Morogoro tumeweza kushirikiana na Kampuni ya Simu ya Itel katika kufanikisha shughuli hii na wadau wengine  ikiwemo Shree Jalalam  katika kuwasaidia mahitaji mbalimbali na kuwarudisha katika furaha makundi hayo,"alisema.


Akitaja vitu walivyowakabidhi watoto hao ni pamoja na Mchele,Unga ,Mafuta ya Kula,Maharage,Taulo za Kike Sabuni ya Unga,Maji,Juice na Biscuits ambazo zimetolewa na wadau hao ikiwa na lengo la kuisaidia Samaf kufikia watoto waliokatika mazingira magumu.


Alisema Jamii inatakiwa kuendelea kuwatunza watoto hao na kuwaona nao wanahaki kama wengine ili kuweza kurudisha tabasamu kwao.


Kwa Upande wake Meneja uhusiano wa Kampuni ya Itel,Fernando Mfuole alisema kampuni yao ya Itel inaendesha kampeni ya kurudisha fadhira kwa jamii  katika kila kila faida wanayopata katika Shule mbalimbali au katika vituo vya watoto vya kulelea yatima,wanaoishi mazingira magumu au venye watoto wenye ulemavu.


"Tunafanya hivi katika mikoa yote  mahali popote nchini, tunarudisha fadhila kwa jamii hii ni kuhakikisha tunawasaidia watoto waliopo katika makundi haya leo tumeweza kutoa mahitaji mbalimbali yanayohitajika  ili kuweza kurudisha furaha za watoto hawa wa kituo cha Amani na Mihayo mkoani Morogoro,"alisema 


Alisema Itel imeweza kuguswa na kuhakikisha inawafikia katika kuwapatia kile kitu walichobarikiwa katika faida wanayoipata kwenye bidhaa zake.


Naye Msimamizi wa kituo Amani  ,Padri Beatus Msewando aliishukuru Kampuni ya Itel na Samaf kwa msaada huo na kuiomba jamii kujitokeza kusaidia kituo hicho kwani wanakabiliwa na Changamoto mbalimbali kutokana na wingi wa watoto wanaowapokea.


"Katika huduma zetu hizi tunaona wengine wanaletwa hawana ndugu wala pakukaa,kwahiyo tunawasaidia kuishi nao huku tukiwafundisha mambo mbalimbali kama kazi za mikono,ikiwemo kilimo na Uvuvi ili kuwapa nyenzo za kuja kujitegemea,"alisema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com