************
Tamasha la 31 la kimataifa la vitabu Tanzania limeanza leo tarehe 11 hadi tarehe 15 mwezi Oktoba katika viwanja vya Posta Kijitonyama Jijini Dar es salaam ambapo Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imeshiriki pamoja na wachapishaji mbalimbali wa vitabu nchini.
Katika ufunguzi wa tamasha hilo mgeni rasmi Prof Evaristo Liwa ambaye alimwakilisha Waziri wa Elimu ,Sayansi na Teknolojia ambaye amesema kuwa , maonesho haya ni muhimu kwani vitabu ni nyezo muhimu katika suala la ufudishaji na ujifunzaji na kusema kuwa serikali itaendelea kuhamasisha jitihada za usomaji nchini .
Prof.Liwa amesema usomaji wa vitabu unatoa ufahamu na uelewa wenye kutoa maarifa ambayo yanaishi ambapo amesisitiza kuwa serikali itaendelea kutambua umuhimu wa uchapishaji nchini .
‘’Usomaji wa vitabu ni jambo muhimu sana nchini hivyo tamasha hili ninaamini litasaidia katika kuendelea kuhamasisha usomaji wa vitabu kwa lengo la kupata maarifa " amesema Prof. Liwa.
Hata hivyo ameeleza kuwa kwa sasa Wizara iko kwenye mchakato wa maboresho ya Sera ya Elimu na Mitaala ambapo baada ya maboresho hayo itaaandaliwa uandishi wa vitabu ambayo itafanyika kwa ushirikiano wa serikali na waandishi binafsi ambavyo vitaweza kutumika katika shule nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TET ,Dkt.Aneth Komba amesema kuwa wataendelea kuungana na sekta binafsi katika kuhakikisha usomaji wa vitabu unakuwa kwa kiasi kikubwa nchini.
‘Tunasisitiza usomaji wa vitabu vyote kila mwanafunzi vya kiada na ziada kwani anapojisomea vitabu tunajenga taifa lenye maarifa katika kujenga nchi yetu tunashirikiana na katika kuamsha ari mpya ya usomaji na tutaendelea kuhimiza ari ya usomaji wa vitabu, tusome vitabu vyote kwa ajili ya kupata maarifa’’ amesema Dkt.Komba
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha wachapishaji nchini(PATA) Bwana Gabriel Kitua amesema kuwa ,tamasha hili litasaidia katika uhimizaji wa usomaji wa vitabu nchini na kwamba kwa kupitia vitabu masuala muhimu kama maadili yanapatikana na kufanya ufahamu mkubwa katika usomaji wa vitabu.
Tamasha hilo linawakutanisha wachapishaji mbalimbali na wananchi wa kawaida ambao watapata nafasi ya kusoma vitabu mbalimbali vinaoneshwa kwenye maonesho hayo.