Afisa Uhusiano Tanesco Mkoa Dodoma Sarah Libogoma ,akizungumza na wananchi wa Kata ya Nala Mtaa wa Seguchini Mkoani Dodoma wakati wa kampeni ya uelimishaji juu ya huduma za TANESCO zilizofika mitaa hiyo kupitia mradi wa umeme wa REA.
WANANCHI wa Mtaa wa Seguchini wakimsikiliza Afisa Uhusiano Tanesco Mkoa Dodoma Sarah Libogoma wakati akitoa kampeni ya uelimishaji juu ya huduma za TANESCO zilizofika mitaa hiyo kupitia mradi wa umeme wa REA Kata ya Nala Mtaa wa Seguchini Mkoani Dodoma.
Afisa usalama Tanesco Mkoa wa Dodoma Ndg Madega dudu,akitoa elimu juu ya huduma za TANESCO zilizofika mitaa hiyo kupitia mradi wa umeme wa REA Kata ya Nala Mtaa wa Seguchini Mkoani Dodoma.
Diwani Kata ya Nala Julius Chimombo akizungumza na Wananchi Mtaa wa Seguchini Kata ya Nala Baada ya Shirika la umeme Mkoa wa Dodoma kwenda kutoa elimu juu ya huduma za TANESCO zilizofika mitaa hiyo kupitia mradi wa umeme wa REA.
...........................................
Na Alex Sonna-DODOMA
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) linaendelea na kampeni ya uelimishaji kata za Dodoma juu ya taratibu za upatikanaji huduma kwa Wateja maeneo yote ya Jiji na usalama wa umeme ikiwemo ulinzi shirikishi wa miundo mbinu ya umeme na umuhimu wake katika shughuli za uzalishaji mali na matumizi ya kawaida ya nyumbani.
Afisa Uhusiano Tanesco Mkoa Dodoma Sarah Libogoma akizungumza na wananchi wa Kata ya Nala Mtaa wa Seguchini Mkoani Dodoma katika kampeni ya uelimishaji juu ya huduma za TANESCO zilizofika mitaa hiyo miezi ya karibuni kupitia mradi wa umeme wa REA.
Amesema wiki hii wamekuwa katika mitaa yote ya Kata ya Nala na kukamilisha kampeni hiyo ya elimu katika mtaa wa Seguchini huku lengo likiwa ni Wananchi kutambua taratibu za huduma, tahadhari juu ya vishoka na Uhujumu miundombinu.
"Ni vyema kila Mtu aelewe na kutambua taratibu zetu za huduma ikiwemo maombi ya umeme na utoaji taarifa, pia kuwapa angalizo na tahadhari juu ya vishoka na wale wanao hujumu miundombinu, jambo ambalo linajitokeza sana kwenye kata yetu hii", amesema
"Tumeona tuendelee kuwakumbusha Wananchi kuwa wanawajibu wa kulinda miundo mbinu na ulinzi ni wa kwetu wote sio wa viongozi tu au wa TANESCO peke yao kwasababu bila hivyo wanaoathirika zaidi ni Wateja na Wananchi kwa ujumla watumiaji umeme eneo husika". Amesema Libogoma
Hata hivyo Afisa usalama Tanesco Mkoa wa Dodoma Ndugu Madega dudu amesema wamekuwa katika kipindi kigumu na Watu wanaohujumu miundo mbinu ya Umeme.
"Uharibifu mkubwa unaofanywa wanaenda kwenye maeneo yanayofungwa mashine umba (Transformer ) na kukata nyaya za mfumo wa kulinda mashine hizo na kusababisha kukosekana huduma ya umeme maeneo mengi vitendo hivi vinaongezeka na hivyo pamoja na kukamata inabidi kuendelea kutoa elimu hii ya tahadhari kwani hili ni la Uhujumu", amesema Dudu
Katika mikutano hiyo ameongezea kwa kutoa rai kwa Wananchi waliofikiwa na wale ambao bado kwa pamoja wawe walinzi katika maeneo yao kwa kutoa taarifa kwa uongozi mtaa husika, polisi kata au kwa shirika la umeme Mkoa wa Dodoma pale wanaposhuhudia vitendo hivyo vya uharibifu wa miundombinu ya umeme inapotokea ikiwemo uchomaji nguzo na hivyo kuepuka athari kubwa kutokea katika mitaa yao kutokana uhujumu huo.
Mtendaji wa Mtaa wa Seguchini Stanley Obedi Msaga amesema wamefurahia kupokea elimu hiyo kutoka kwa Shirika la Umeme Mkoa wa Dodoma na Wananchi sasa wanaendelea na taratibu za uombaji pamoja na Ofisi kuwasilisha taarifa na majina ya wahitaji walio mbali na miundombinu kuweza kufikiwa pia.
"Kimsingi Tumewaelewa vizuri TANESCO na tunawashukuru kwa kuturahisishia upatikanaji huduma kupitia Mfumo wao wa Nikonekt ambao umeshatatua changamoto nyingi zilizokuwepo awali hivyo nasi tutaendeleza kutoa ushirikiano kwao ili kuweza kutokomeza hujuma zinazoweza kujitokeza kwenye miundombinu ya maeneo yetu kwani umeme huu serikali imelenga uwe ni wa maendeleo zaidi kwenye mitaa yetu", amesema Msaga.
Mkutano huo ulihusisha mitaa ya Segu Juu, Bwawani na wenyeji wa kikao mtaa wa Seguchini ambapo pia ulihudhuriwa na Mstahiki Meya Prof. Davis G Mwamfupa pamoja na Diwani wa kata hiyo ambapo uhamasishaji uchangiaji jitihada za maendeleo ya Kata ulifanyika pia.