Katibu wa Tume ya Utumishi wa walimu (TSC)Mwl.Paulina Nkwama. |
Na Dotto Kwilasa,DODOMA.
TUME ya Utumishi wa Walimu (TSC) imeitaja mafanikio iliyopata katika uongozi wa serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwa ni pamoja na kuajiri walimu 16,749 wakiwemo 8,949 wa shule za msingi na 7,800 wa shule za sekondari.
Akizungumza na wandishi wa habari leo Oktoba 27,2022 Katibu Ofisi ya Rais, Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC) Mwalimu Paulina Nkwama amesema walimu 15,802 wamesajiliwa ambapo kati yao walimu wa shule za msingi walikuwa 8,512 na Sekondari walikuwa 7,290.
“Walimu 6,949 sawa na asilimia 100 walithibitishwa kazini wakiwemo 3,949 wa Shule za Msingi na 3,000 wa shule za sekondari,”amesema
Licha ya hayo amesema pamoja na jitihada za kutoa elimu bado kuna walimu ambao wamekuwa hawazingatii Miiko na Maadili ya kazi yao ambapo katika kipindi cha mwezi Machi mwaka jana hadi Septemba mwaka huu jumla ya Walimu 1,952 walifunguliwa Mashauri ya kinidhamu huku kati yao 919 walifukuzwa kazi kutokana na utoro, ulevi,kugushi vyeti na mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi.
Amesema walimu wenye tabia hizo hufikishwa katika mamlaka za kinidhamu kwa ajili ya kushughulikiwa kwa kuwachukulia hatua za kinidhamu ili kuwanusuru watoto kupata huduma ya elimu iliyokusudiwa na Taifa.
“Katika kipindi cha Machi mwaka jana hadi Septemba mwaka huu walimu 1,952 walifunguliwa mashauri ya kinidhamu katika mashauri hayo 1,362 sawa na asilimia 69.8 ya mashauri yote yalihusu utoro,mashauri 260 sawa na asilimia 13.3 ya mashauri yote yalihusu kughushi vyeti, 119 yalihusu mahusiano ya kimapenzi na wanafunzi, 98 yalihusu ukaidi, 66 sawa na asilimia 3.4 yalihusu ulevi, 16 sawa na asilimia 0.8 yalihusu ubadhirifu na mashauri 31 sawa na asilimia 1.6 yalihusu makosa to mengineyo,"amesema.
Amefafanua kuwa mashauri 1,642 yaliyoamuliwa walimu 919 sawa na asilimia 56 ya adhabu zilizotelewa walifukuzwa kazi, walimu 234 sawa na asilimia 14.3 hawakupatikana na hatia, walimu 115 sawa na asilimia saba ya adhabu zilizotolewa walishushwa cheo.
Amesema walimu 89 sawa na asilimia 5.4 walikatwa mshahara asilimia 15 kwa muda wa miaka mitatu, Walimu 143 sawa na asilimia 8.7 walipewa adhabu ya Karipio, Walimu 59 sawa na asilimia 3.6 walipewa adhabu ya onyo na walimu 77 sawa na asilimia 4.7 walipewa adhabu ya kufidia hasara.
Kuhusu kupanda madaraja Mwalimu Nkwama amesema kuwa katika kipindi cha nyuma kilio kikubwa cha walimu kilikuwa ni kucheleleweshwa kupanda vyeo na kwamba zoezi hilo sasa hufanywa kwa kushirikiana na waajiri katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora
“Walimu 47,158 walipandishwa cheo kati yao 22,943 ni wa shule za msingi na 11,524 wa sekondari kwa mwaka huu wa fedha huku walimu 12,546 walibadilishiwa vyeo baada ya kujiendeleza kielimu,”amesema
Social Plugin