Mkurugenzi wa Biashara wa Jumuisha ya Afrika Mashariki (EAC), Rashid Kibowa amesema kuwa moja ya changamoto inayowakabili wafanyabiashara wa EAC ni kuzalisha bidhaa zenye ubora wa chini.
Kauli hiyo ameitoa jana Oktoba 20 jijini Dar es Salaam wakati wa utoaji wa tuzo za ubora za Afrika Mashariki kwa mwaka 2022 , hafla ambayo imefanyika katika hoteli ya four point.
Amesema changamoto hiyo inafanya biashara za wafanyabiashara wengi katika ukanda huu zisivuke mipaka ya jumuiya hiyo na hivyo kushindwa kushindana na wafanyabiashara wengine wa Afrika na kimataifa.
“Tunatakiwa kujiimarisha ili kushindana na watu wengine duniani,” amesema Kibowa.Kibowa amesema kuna muamko mkubwa wa wajasiriamali kuzalisha bidhaa ili kujipatia kipato lakini wengi wao hawana ujuzi na maarifa yanayowawezesha kuzingatia viwango vya ubora vya kimataifa.
Amesema Wafanyabiashara Afrika Mashariki wanatakiwa kuzalisha bidhaa na kutoa huduma zenye ubora na viwango ili kufaidika zaidi na soko la kimataifa lenye faida lukuki.
Aidha amesema Miongoni mwa masoko muhimu la kimataifa kwa wajasiriamali ni Eneo la Biashara Huria la Afrika (AfCFTA) ambalo ni makubaliano ya biashara huru ya Afrika kati ya nchi 54 wanachama wa Umoja wa Afrika (AU).
Kutokana na hali hiyo, nchi za EAC zinaagiza zaidi bidhaa mbalimbali kutoka nje na kulazimika kusafirisha malighafi kama mazao ya kilimo ili yakachakatwe nje na kurejeshwa tena katika nchi zao.
Pamoja na hayo amesema kuna umuhimu wa kuwajengea uwezo wafanyabiashara na wajasiriamali wakubwa kwa wadogo katika michakato yao yote ya utengenezaji bidhaa kuhakikisha suala la viwango vya ubora haliachwi nyuma. Njia nyingine itakayosaidia wazalishaji wa bidhaa kushindana na wenzao wa Afrika na kimataifa ni kuwaondolea vikwazo mbalimbali ikiwemo kodi na masharti magumu ya kusafirisha bidhaa kutoka nchi moja kwenda nyingine.
Frank Dafa, Meneja Sera za Viwango wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC) amesema katika jumuiya hiyo wanaendelea kuondoa vikwazo vinavyowarudisha nyuma wafanyabiashara na kuwafungulia fursa za kufaidika na masoko ya bidhaa ya kimataifa.
“Afrika Mashariki tumekuwa na hatua mbalimbali zinazochukuliwa kuweka mifumo ya kuoanisha sheria zetu za bidhaa ili kuhakikisha haziwi kikwazo kwenye biashara,” amesema Dafa.
Social Plugin