Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MKENDA AIONYA BODI YA MIKOPO

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda 

Na Mwandishi wetu,WEST-Dar es salaam.

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda ametoa onyo kwa uongozi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kutokana na kitendo cha bodi hiyo  kutotoa ushirikiano kwa kamati ya kuchunguza utoaji wa mikopo.

Waziri Mkenda ametoa onyo hilo jana tarehe Octoba 25, 2022 wakati akizungumza na waandishi wa habari Jijini Dar es salaam na kusema kuwa Bodi inasuasua kutoa ushirikiano kwa kamati aliyoitangaza tarehe 31 Julai mwaka huu alipotembelea ofisi za Bodi hiyo maeneo ya Tazara Jijini Dar es salaam.

Waziri Mkenda ameeleza kuwa majukumu aliyoyatoa kwa kamati hiyo ilikuwa ni kuchunguza uhalali katika utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2017/2018 mpaka 2021/2022 ili kubaini kama kulikuwa na upendeleo wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wasiokuwa na sifa zilizoainishwa.

Amesema;"nitakula kichwa cha mtu kama Bodi ya Mikopo itaendelea kusuasua katika utekelezaji wa kazi hii,mmekuwa mkisua sua mara mpite huku mara mtokee huku Lengo la timu hii tungependa kile kidogo tulichonacho kitolewe kwa haki kusaidia wale wenye mahitaji makubwa zaidi"amesema Prof Mkenda na kuongeza;

“Lazima mhakikishe kwamba hakuna upendeleo,hakuna kutoa fursa Kwa kuangaliana mfano mtoto wangu au ndugu zangu wenye uwezo kuhakikisha wao wanapata kwa sababu wao wana connection wakati mtu ambaye hana connection hapati,” amesisitiza

Waziri Mkenda ameonyesha masikitiko yake dhidi  ya HESLB na kueleza kuwa kamati hiyo imechelewa kufanya kazi yake kwa sababu ya ‘lobbying’ (inashawishi) huku na kule ilihali wakifahamu kwamba kamati ya waziri haisimamishwi kufanya kazi.

“Sisi tunataka kujisahihisha ili kuhakikisha kwamba kile ambacho serikali imetenga kwa ajili ya mikopo kwa wanafunzi kinaenda kwa mlengwa, sasa ninataka kutoa onyo ya kwamba kwenda kulobby sijui eti waziri asimamishe kamati isifanye kazi… hiyo lobbying inaonesha kuna madudu,

“Natuma salamu kwa bodi ya mikopo kwa sababu niliona wamejaribu wanasema ooh tumeitwa sijui tumetuma tusimamishe wakati kazi nimeitoa mimi na mimi ndio nimepewa kazi ya kusimamia mikopo.

“Bungeni watu wanalalamika sana, wanasema kuna yatima hawapewi mikopo, alafu watu wenye uwezo wanapewa mikopo, mimi naunda kamati alafu nisikie kuna mtu anasema waziri asiunde kamati, aah! Nitakula kichwa cha mtu,” amesisitiza

Aidha Kamati hiyo ya kufuatilia utoaji wa mikopo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2017/2018 mpaka 2021/2022 aliyoitangaza Waziri Mkenda, inaongozwa na Profesa Allan Mushi ambaye ni mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe Morogoro, Idd Makame kutoka Zanzibar na Dk. Martin Chegeni ambao wote kwa pamoja ni wataalamu wa mifumo waliobobea katika sayansi ya kompyuta na takwimu.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com