JENISTA ATOA WITO KWA WATUMISHI WA UMMA KUTUMIA MFUMO WA eMREJESHO KUWASILISHA MALALAMIKO YAO

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Kilimanjaro, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Kilimanjaro iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.

Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Kilimanjaro, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Waziri huyo mkoani Kilimanjaro iliyolenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao.


Afisa Tarafa Kata ya Moshi Magharibi, Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, Bw. Senzia Lushino akiwasilisha hoja kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama wakati kikao kazi cha Waziri huyo na Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Kilimanjaro, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi kilicholenga kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi wa mkoa huo.

***********************

Na. Veronica Mwafisi - Moshi

Tarehe 14 Oktoba, 2022

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Jenista Mhagama ametoa wito kwa watumishi wa umma nchini kutumia mfumo wa kielektroniki wa ushughulikiaji wa malalamiko ya watumishi wa umma na wananchi katika utumishi wa umma (eMrejesho) kuwasilisha malalamiko yao ambayo yamechukua muda mrefu kufanyiwa kazi na waajiri wao ili yaweze kufanyiwa kazi kwa wakati na kuwawezesha watumishi hao kutekeleza majukumu yao kikamilifu.

Mhe. Jenista ametoa wito huo kwa watumishi wa umma wote nchini wakati akizungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Kilimanjaro, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi na Halmashauri ya Wilaya ya Moshi akiwa kwenye ziara ya kikazi ya mkoani Kilimanjaro.

Mhe. Jenista amesema, mfumo wa eMrejesho ni mfumo pekee unaochangia ushughulikiaji wa malalamiko kwa wakati na kuuboresha utumishi wa umma kuwa uliotukuka, hivyo watumishi wa umma wanapoona malalamiko yao yanachelewa kufanyiwa kazi katika vituo vyao vya kazi, wayawasilishe Ofisi ya Rais-UTUMISHI kupitia mfumo huo.

Katika kuhakikisha watumishi wanawasilisha malalamiko yao kupitia mfumo huo, Waziri Jenista amewasisitiza Watendaji Serikalini kutoa taarifa kwa watumishi wa umma wote juu ya uwepo wa mfumo huo ili wautumie katika kutatua changamoto zinazowakabili.

“Katibu Tawala nikuombe sana kuhakikisha watumishi katika halmashauri zote wanapewa taarifa za mfumo wa eMrejesho ili waufahamu na kuweza kuutumia kwa kuwasilisha malalamiko yao, maoni na hata ushauri ili kuujenga utumishi wa umma,” Mhe. Jenista amesisitiza.

Mhe. Jenista ameongeza kuwa mfumo huu umetengenezwa sio kwa ajili ya matumizi ya watumishi wa umma pekee bali hata kwa wananchi ambao wanaweza kuutumia kwa kuwasilisha changamoto zilizo katika maeneo wanayoishi akitolea mfano migogoro ya ardhi na uhaba wa maji kwani kwa kufanya hivyo kutawapunguzia Viongozi Wakuu wa Kitaifa kadhia ya kushughulikia malalamiko wanapokuwa katika ziara zao za kikazi kwani yatakuwa yameshughulikiwa na maafisa husika katika taasisi.



Pamoja na uwepo wa mfumo wa eMrejesho, Mhe. Jenista amesema akiwa ndiye Waziri anayemsaidia Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kusimamia utumishi wa umma na utawala bora anao mfumo unaojulikana kwa jila la SEMA NA WAZIRI WA UTUMISHI ambao umeunganishwa na dawati la huduma kwa mteja ukilenga kutatua changamoto za kiutumishi na utawala bora.



Mhe. Jenista amefanya kikao kazi na watumishi wa mkoa wa Kilimanjaro ikiwa ni utaratibu aliojiwekea wa kukutana na watumishi wa umma nchini kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji na kutatua changamoto zinazowakabili watumishi hao ili waweze kutoa huduma bora kwa wananchi kwa ustawi wa taifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post