Watu wawili wamefariki dunia na wengine watatu kujeruhiwa katika ajali iliyohusisha magari manne likiwemo basi la abiria la Kampuni ya Mangare Express lenye namba za usajili T 601 DCX linalofanya safari zake kati ya Mbeya na Sumbawanga.
Taarifa iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga imeeleza kuwa ajali hiyo imetokea majira ya saa 12:45 asubuhi ya leo katika eneo la Mlima Iwambi nje kidogo ya Jiji la Mbeya katika barabara kuu ya Mbeya kwenda Tunduma.
Amesema chanzo cha ajali hiyo, ni basi hilo kuligonga gari namba T.452 DHD Toyota Raum na kusababisha vifo vya watoto wawili waliokuwa ndani ya gari hilo.
Ameendelea kueleza kuwa baada ya gari hilo kuligonga gari dogo, liliendelea kugonga gari jingine lenye namba za usajili T.673 DMV lenye tela namba T.362 DMG aina ya Scania lililokuwa linaelekea Mbeya na gari namba DAD 3981 na tela lake ABF 75591 aina ya Dofeng.
Kamanda Kuzaga amesema chanzo cha ajali ni mwendo kasi katika eneo lenye mteremko mkali ambapo majeruhi wanaendelea kutibiwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya huku jitihada za kumtafuta dereva aliyetoroka zikiendelea.
Social Plugin