Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limewakamata watu watano wanaodaiwa kuhusika na mauaji kijana Joseph Mathias (38) ambaye ni mlemavu wa Ngozi [Albino) mkazi wa Kijiji cha Ngula wilaya ya Kwimba mkoani Mwanza huku mmoja akikutwa na mkono wa mtu huyo ndani ya begi akisaka mganga amuuzie.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza Wilbroad Mutafungwa amesema baada ya tukio hilo kutokea Novemba 2/2022 Polisi walianza msako mara moja wa kuwabaini waliohusika na mauaji hayo ndipo wakafanikiwa kuwakamata watu watano akiwemo mwanaume mmoja ambae jina limehifadhiwa aliyekamatwa wilayani Misungwi akiwa na begi jeusi lililokuwa na kitu ndani kilichokuwa kinatoa harufu ndipo wananchi wakashtuka na kuwaita polisi walipompekua wakakuta mkono wa mtu ndani ya begi hilo
"Mtuhumiwa huyo bado anaendelea kutoa ushiikiano kwa jesho la polisi na kupelekea watuhumiwa wengine kukamatwa huku wengine wakiendelea kutafutwa na upelelezi bado unaendelea kufanyika ukikamilika yeye na watuhumiwa wenzake watafikishwa mahakamani", amesema.
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi Mwanza linawashikilia watu 14 akiwemo Diwani wa kata ya Buzilasoga Daudi Shilinde na Mwenyekiti wa CCM Kijiji cha Ikoni B na kamanda wa sungusungu kwa mauaji ya kumshambulia na kumchoma moto mama mmoja aitwaye Getrude Dotto wakimtuhumu kosa la wizi wa mihogo.
"Watu hao pamoja na viongozi wao walishirikiana kwa Pamoja wakamshambulia kwa fimbo na marungu na hatimaye walikusanya majani Pamoja na vipande vya miti na kumchoma moto pia walichoma nguo za mama huyo aliyekuwa akiishi na Watoto wake wawili na kubomoa nyumba yake pia", amesema Kamanda Mutafungwa
Na katika tukio lingine Kamanda Mutafungwa ameongeza kuwa Pendo Embasy mwenye umri wa miaka 28 anashikiliwa kwa tuhuma za kuiba mtoto wakiume mwenye umri wa miezi sita.
CHANZO - EATV