Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

BENKI YA CRDB YAZINDUA MFUMO MPYA WA MAWAKALA , SASA WATAWEZA KUFUNGUA AKAUNTI NA KUTOA KADI


Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye (kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (katikati) pamoja na Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa, wakipiga makofi wakati wa uzinduzi rasmi mfumo mpya na wakisasa utakaowawezeza mawakala wa benki hiyo kutoa huduma kwa urahisi zaidi kupitia simu janja zao, uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es salaam, Novemba 15, 2022.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye (katikati) akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, wakati wa uzinduzi rasmi wa mfumo mpya na wakisasa utakaowawezeza mawakala wa benki ya CRDB kutoa huduma kwa urahisi zaidi kupitia simu janja zao, uzinduzi huo uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es salaam, Novemba 15, 2022. Kulia ni Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa.
Benki ya CRDB imekamilisha na kuuuzindua mfumo mpya na wakisasa utakaowawezesha mawakala wake zaidi ya 25,000 waliopo nchi nzima kumfungulia mteja akaunti na kumpa kadi ndani ya muda mfupi ili afurahie huduma za benki, imefanya hivyo kwa kutambua mchango wa mawakala katika kusogeza huduma za benki karibu zaidi na wananchi hususani waliopo maeneo ambayo hayana matawi ya benki.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mfumo huo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alisema sekta ya fedha ina mchango mkubwa katika ukuaji na maendeleo ya uchumi, kujenga uchumi jumuishi, na kupunguza umasikini ndio maana Serikali nyingi duniani kote zinatilia mkazo suala la ujumuishi wa kifedha (financial inclusion).

"Hapa nchini Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kisera ili kukuza ujumuishi wa kifedha kwa wananchi, Baadhi ya jitihada za kisera na kimkakati ambazo zimefanyika ni pamoja na kuanzishwa kwa Mpango wa Elimu ya Kifedha (Financial Education Program 2021/22 – 2025/26) na mwaka 2020, Serikali ilizindua Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha (Financial Sector Development Master plan - 2020/21 -2029/30)," alisema Nnauye.



Pamoja na juhudi hizo, Waziri Nnauye alisema bado idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za benki ni ndogo akikumbusha utafiti wa kwanza wa Finscope wa mwaka 2006 ulioonyesha kuwa ni asilimia 46 tu ya watu wazima walijumuishwa kifedha, ambapo asilimia 11 tu walikuwa wakitumia huduma rasmi za kifedha.
Sababu kuu za watu wengi kuwa nje ya mfumo wa fedha, alisema ni ufikiwaji mdogo wa huduma za benki kupitia matawi katika maeneo ya vijijini na gharama kubwa za ufikiaji wa huduma za kifedha ikiwemo hitaji la kusafiri umbali mrefu katika maeneo yenye matawi ya benki kwani nyingi zilikuwa maeneo ya mkoani au wilayani.


Kwa kutambua mchango wa teknolojia kutatua changamoto hiyo, alisema Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Februari 2013 ilitoa Mwongozo wa Huduma za benki kupitia wakala na leo hii Benki ya CRDB ina zaidi ya mawakala 25,000 ambao ni sawa na asilimia 46 ya mawakala wote 55,000 wa benki waliopo nchini wanaofanikisha zaidi ya miamala milioni 100 yenye thamani ya shilingi trilioni 50 zikiwamo shilingi trilioni 1.3 za mapato ya Serikali.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema, CRDB ndiyo ilikuwa Benki ya kwanza nchini kuanzisha huduma kupitia mawakala mwaka 2013 ikiwasajili mawakala 500 na leo hii inajivunia kuwa nao zaidi ya mawakala 25,000 ambao wamesambaa kote nchini hivyo kuifanya iongoze nchini na kuwa ya tatu Afrika Mashariki.


"Mfumo wa CRDB Wakala umekua na mchango mkubwa katika ufikishaji wa huduma za fedha kwa wananchi, taarifa zetu za utendaji zinaonyesha zaidi ya miamala milioni 100 yenye thamani ya shilingi Trilioni 50 imekua ikifanyika kupitia CRDB Wakala kwa Mwaka, mfumo huu pia umekua ukisaidia katika ukusanyaji wa mapato ya serikali ambapo takribani Trilioni 1.3 hukusanywa kwa mwaka," alisema Nsekela.
Aidha, Nsekela alifafanua kwamba mfumo huo wa CRDB Wakala unatoa huduma za fedha kwa watanzania milioni 3 kwa mwezi ambapo asilimia 40 ni wateja wa Benki na asilimia 60 ni wananchi wengine.


Mfumo wa CRDB Wakala, alisema umetoa zaidi ya ajira 35,000 kwa vijana wanaopokea kamisheni kwa miamala wanayoifanya.


CRDB Wakala App ni mfumo mpya wa kisasa, salama na wa kidijitali unaotumika kwenye simu janja kutoa huduma za kibenki kwa ufanisi wa hali ya juu hivyo kuongeza ufanisi, kasi ya utoaji huduma na kupunguza gharama za uendeshaji kwa watoa huduma hasa kwa mawakala wa Benki.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akibonyeza sehemu yenye ujumbe wa Ubora wakati wa uzinduzi rasmi wa mfumo mpya na wakisasa utakaowawezeza mawakala wa benki ya CRDB kutoa huduma kwa urahisi zaidi kupitia simu janja zao, uzinduzi huo uliofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es salaam, Novemba 15, 2022. Wanaoshuhudia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (katikati), Afisa Mkuu wa Fedha wa Benki ya CRDB, Fredrick Nshekanabo (watatu kushoto), Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa (kushoto) pamoja na Mkuu wa Kitengo cha Masoko wa Benki ya CRDB, Joseline Kamuhanda.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com